IQNA

Spika wa Bunge la Iran

Dunia iishinikize Marekani iondoe vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran ili Corona iangamizwe

15:53 - March 10, 2020
Habari ID: 3472550
TEHRAN (IQNA) - Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran yaani Bunge ameandika barua kwa Umoja wa Mabunge na Maspika wa Mabunge ya Nchi mbalimbali duniani na kuitaka jamii ya kimataifa kupaza sauti kwa pamoja ili kuondolewa haraka iwezekanavyo vikwazo vikiwemo vya kitiba vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran.

Ali Larijani leo Jumanne ameandika barua tofauti kwa Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kiislamu OIC, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Asia na pia kwa Maspika wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu na za Asia na kueleza kusikitishwa na vikwazo dhidi ya binadamu vya Marekani dhidi ya Iran. Dakta Larijani amesema hatua za Washington vikiwemo vikwazo vya kitiba, dawa na vifaa vya maabara zinazuia kutokomezwa maambukizo ya virusi vya corona.  

Larijani amesisitiza kuwa kitendo cha Marekani cha kuweka vikwazo kinakinzana waziwazi na hati za Umoja wa Mataifa na Matamko ya Shirika la Afya Duniani; na kina taathira hasi na zisizokubalika kwa jitihada zote za kitaifa, kieneo na kimataifa kwa ajili ya kudhibiti na kutokomeza maambukizo ya virusi vya corona.  

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia namna WHO lilivyotangaza hali ya hatari katika baadhi ya nchi kutokana na mlipuko wa corona na kuongeza kuwa, hali ya mambo hii leo kimataifa kuliko wakati mwingine wowote ule imepelekea kuwepo ulazima wa kufanywa juhudi na kushirikiana kitaifa, kieneo na kimataifa ili kukusanya suhula zote za kiufundi na kilojistiki ili kuzisaidia nchi zilizoathiriwa na virusi hivyo tajwa.  

Mlipuko wa virusi vya corona ulianza mwezi Disemba mwaka jana katika mji wa Wuhan China; na inaonekana kuwa chanzo cha maambukizo ya virusi hivyo ni wanyama wasiofugwa nyumbani. 

Maambukizo ya corona yameshaziathiri sasa nchi 115 ikiwemo China. Aidha zaidi ya watu 115,000 duniani wameambukizwa virusi hivyo; ambapo miongoni mwao zaidi ya watu elfu 64 wamepona na zaidi ya elfu nne wengine wamepoteza maisha. 

3884352

captcha