IQNA

Rais wa Iran katika ujumbe maalumu wananchi wa Marekani
19:31 - March 21, 2020
News ID: 3472588
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia ujumbe maalumu wananchi wa Marekani akitahadharisha kuwa: Siasa zozote za uono finyu na za uhasama zitazolenga kudhoofisha mfumo wa utabibu na kuviwekea mpaka vyanzo vya fedha vya kushughulikia hali mbaya iliyoko Iran zitakuwa na athari ya moja kwa moja kwa mchakato wa kupambana na janga la dunia nzima la corona katika nchi zingine.

Katika ujumbe huo aliotuma usiku wa kuamkia leo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, vikwazo vya serikali ya Marekani vimeathiri siha za raia wengi wa kawaida wa Iran mbali na kuwapotezea vipato na ajira zao. Hata hivyo amesisitiza kuwa: Mara hii pia wananchi wa Iran, watamudu kwa muqawama na heshima kukabiliana na kirusi, vikwazo au sera za kidhalimu na stratejia ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya serikali ya sasa ya Marekani.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Rais Rouhani amesisitiza pia kwamba, taifa la Iran litakivuka kipindi hiki kigumu na akaongezea kwa kuhoji: Hivi kweli wananchi wa Marekani wanaridhia watu wa Iran wahimili mashinikizo haya ya kidhalimu yanayowekwa kwa niaba yao, kura zao na kodi zao wanazolipa?

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile amesema, wakati umefika kwa wananchi wa Marekani kupaza sauti zao kwa kuhoji na kutaka majibu kwa serikali yao na akawahutubu kwamba: Msikubali nyaraka za historia ya Marekani zizidi kuwa chafu zaidi ya hivi.

Licha ya kuenea maambukizo ya kirusi angamizi cha corona duniani ikiwemo nchini Iran pamoja na ulazima wa kupambana nacho mtawalia na kwa kila hali, Marekani ingali inang'ang'ania mtazamo wake wa kuendeleza vikwazo dhidi ya Iran kupitia sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa huku ikiendelea kila mara kutangaza vikwazo vingine vipya dhidi ya Tehran.

3886692

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: