IQNA

Maeneo ya ibada kufunguliwa Kenya baada ya kufungwa kutokana na COVID-19

20:38 - July 07, 2020
Habari ID: 3472938
TEHRAN (IQNA) – Serikali ya Kenya imetangaza kuwa maeneo ya ibada yatafunguliwa tena nchini humo lakini kwa sharti la kuzingatia kanuni na sheria maalumu za kuzuia kuenea ugonjwa wa COVID-19 au corona.

Akizungumza Jumatatu, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema maeneo ya ibada yametakiwa yasiwe na waumini wasiozidi 100 katika kila ibada itakayofanyika na ibada zitafanyika si zaidi ya kipindi cha saa moja.

Sheria zingine zilizowekwa ni kuwa ni sharti maeneo hayo ya ibada yawe na sehemu maalumu za kunawa mikono au zenye dawa za kupaka mikono zenye uwezo wa kuua virusi vya corona. Aidha waumini wanatakiwa kuvaa barakoa au maski wakati wote na wadumishe umbali wa mita 1.5 baina ya kila mtu wakiwa ndani ya maeneo ya ibada. Halikadhalika watakaoruhusiwa kuingia katika maeneo ya ibada ni wale wenye umri wa baina ya miaka 13 hadi 58. Aidha maeneo ya ibada yanawajibika kusafishwa kwa kemikali za kuua virusi mara kwa mara na kupima kiwango cha joto mwilini cha waumini.

Kwa mujibu wa Baraza la Wafuasi wa Dini Mbali Mbali Kenya, maeneo ya ibada ikiwemo misikiti, makanisa na mahekalu, yatafunguliwa kuanzia Julai 14.

Hatahivyo mafunzo ya Shule za Jumapili za watoto Wakristo na Madrassa za Waislamu zitaendelea kufungwa mpaka maelekezo mengine yatakapotolewa. 

Rais Kenyatta ametangaza kuwa safari za ndege ndani ya Kenya zitaanza tena tarehe 15 mwezi Julai mwaka 2020; kwa kuzingatia miongozo na kanuni kutoka kwa wataalamu wa afya kutoka wizara ya afya na mamlaka ya usafi wa anga nchini humo.

Safari za kimataifa za kuingia na kutoka nchini zitaanza tarehe 1 mwezi Agosti 2020.

3909253

captcha