IQNA

Imam Mahdi (ATF), Mwokozi wa Dunia Anayesubiriwa

15:28 - April 07, 2020
Habari ID: 3472641
TEHRAN (IQNA)- Tarehe 15 Shaaban Hijiria Qamaria ni kumbukumbu ya kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu, Imam Mahdi –Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake- (ATF).

Nuru ya umaanawi ya uwepo wa Imam Mahdi ATF imeenea hata katika wakati huu wa "ghaiba" au kutokuwepo mtukufu huyo machoni mwa walimwengu.

Kabla ya kumuumba mwanadamu, Mwenyezi Mungu aliwaambia Malaika wake: 'Na pale Mola wako alipowaambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (al-Baqarah:30). Khalifa wa kwanza alikuwa Nabii Adam (as) na baada yake wakaja Manabii na Mawalii Wake wengine. Kuwepo kwa khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi ni moja ya Sunna zake zisizobadilika, ambayo itaendelea kuwepo hadi mwisho wa dunia. Khalifa huyu ni dhihirisho halisi la haki na ana mawasiliano na Mwenyezi Mungu kuliko mtu mwingine yeyote.

Khalifa wa Mwenyezi Mungu

Mwanadamu akiwa ni khalifa wa Mwenyezi Mungu anayeakisi na kuwasilisha ukamilifu na haki ya Mungu Muumba katika ardhi, ndiye kiumbe bora zaidi duniani. Katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani, Mwenyezi Mungu anahadithia visa vya kaumu mbalimbali na jinsi alivyowachaguliwa Manabii na makhalifa waliopasa kuwaongoza kwenye njia nyoofu. Baadhi ya kaumu hizo ziliwakubali Manbii hao hali ya kuwa nyingine ziliwakataa na kuwakadhibisha, jambo lililozipelekea kuadhibiwa na kuangamizwa na Mwenyezi Mungu. Visa hivyo vina ujumbe mmoja nao ni kwamba kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuiacha kaumu yoyote bila kuichagulia khalifa na huu ndio mfumo jumla wa uumbaji. Imam Ali (AS) pia katika hotuba ya kwanza katika kitabu cha Nahjul Balagha na baada ya kuashiria kuumbwa kwa Adam anasema kuwa kamwe Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuiacha jamii ya mwanadamu bila ya kuichagulia Mitume, kitabu cha mbinguni, hoja ya lazima na njia iliyonyooka.

Hivi sasa pia Imam Mahdi (ATF) akiwa ni khalifa anayemwakilisha Mwenyezi Mungu, anaishi pamoja na sisi humuhumu duniani, hata kama hatuwezi kumuona. Mtukufu huyo alizaliwa huko katika mji wa Samarra, Iraq ya leo,  Alfajiri ya siku ya Ijumaa tarehe 15 Shaaban 255 Hijiria. Alipewa jina sawa na la Mtume (SAW) yaani Muhammad na pia kunia yake ya Abul Qassim. Imam Mahdi (ATF) alichukua ukhalifa wa kuongoza Umma wa Kiislamu mwaka 260 Hijiria kufuatia kuuawa kwa baba yake mpendwa al-Imam Hassan Askari (AS) na kwa mujibu wa Sunna ya moja kwa moja ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa msingi huo alichaguliwa kuhudumia nafasi hiyo muhimu na Mwenyezi Mungu mwenyewe, uongozi ambao bado unaendelea hadi leo hata baada ya kupita maelfu ya miaka.

Ghaiba

Imam Mahadi (ATF) ambaye hivi sasa yuko kwenye ghaiba yaani haonekani machoni pa walimwengu kwa amri ya Mwenyezi Mungu, atadhihiri tena na kuubadilisha kabisa ulimwengu kiuongozi. Atafanya mabadiliko makubwa na kung'oa mizizi yote ya utawala duniani ambayo imesimama kwenye msingi wa dhulma na uonevu. Atabuni utawala mwingine mpya kabisa uliosimama juu ya msingi wa thamani za Mwenyezi Mungu ili ahadi yake Muumba iweze kuthibiti na hivyo amani na upendo uliofungamana na uadilifu uweze kutawala duniani. Maadui wa dini ya Mwenyezi Mugu ambao daima huwa wanaimarisha kufri na kufanya juhudi za kuficha ukweli (Aya ya 5: Surat al-Qasas), mara hii pia na kama ilivyo kawaida yao, walipanga njama ya kutaka kumuua Imam na khalifa huyo wa Mwenyezi Mungu lakini Mungu akamuepusha na shari hiyo kwa kumfanya asionekane machoni pa watu, ili apate kubakia hai na wakati muwafaka utakapofika, atadhihiri tena na kuujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu.

Imam Mahdi ataunda serikali

Imam Mahdi (ATF)  anaona na kushuhudia moja kwa moja matendo na mambo yote wanayoyafanya waumini na wafiasi wake hadi wakati wa kudhihiri kwake hadharani utakapowadia. Kudhihiri kwa Imam huyo wa mwisho, kunahitajia kupita wakati na kukomaa kwa akili, elimu na akhlaqi (maadili) ya watu na kuwa kwao tayari kwa ajili ya kushirikiana naye wakati muwafaka. Imam huyo wa mwisho wa Mwenyezi Mungu atawaongoza wanadamu wote kwenye njia nyoofu kuelekea kwa Muumba wao wakati ambao atapata fursa ya kuunda serikali itakayosimama juu ya misingi ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu, kutekeleza uadilifu na kuheshimu sheria, na bila shaka jambo hilo litawezekana tu wakati wanadamu watakapokuwa tayari kukubali na kufuata miongozo ya mbinguni. La sivyo, iwapo mazingira kama hayo hayatakuwepo kwenye jamii na watu kutokuwa tayari kufuata na kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu kupitia Imam Mahdi (ATF),  kudhihiri kwake miongoni mwa watu wa aina hiyo hakutakuwa na maana wala faida yoyote. Katika maisha yake ya kijamii, mwanadamu anahitajia serikali na mtawala atakayelinda maisha yake na kumfanya apate maendeleo katika nyanja tofauti. Mwanadamu anapasa kuheshimu na kutii amri za watawala ili waweze kubuni jamii bora, salama, yenye utulivu na inayojitenga na kila aina ya dhulma na uonevu. Lakini kwa bahati mbaya hilo halijaweza kuthibiti bali tunayoshuhudia ni kuwa jamii ya mwanadamu inaendelea kukabiliwa kila siku na ongezeko la dhulma na uonevu. Hivyo katika mazingira ya hivi sasa ambapo jamii imetumbukia kwenye lindi la matatizo ya kisiasa na kiusalama, fitina kuenea kila sehemu, magonjwa sugu na yasiyo na tiba kuikumba jamii na utovu wa nidhamu na maadili kuenea kila upande, mwanadamu kwa dhati yake anahisi na kutarajia kuwadia siku ambayo itatawaliwa na mtawala anayefuata thamani na miongozo ya Mwenyezi Mungu, ambaye ataweza kutekeleza na kueneza uadilifu katika jamii.

Matarajio na kusubiri

Matarajio au kusubiri huko ndiyo mazingira yanayofaa kwa ajili ya kukubalika utawala wa ulimwengu wa Imam Mahdi (ATF), ambayo yanapasa kuwa katika kila jamii ya mwanadamu. Ni wazi kuwa tunapasa kuzingatia nukta hii kwamba kusubiri huku hakupasi kuchukuliwa kuwa na maana ya kupuuza mambo na kukaa kimya. Mwanadamu hapasi kuketi pembeni na kutochukua hatua yoyote ya kurekebisha hali ya mambo katika jamii, bali kusubiri kuna maana ya matumaini na matarajio. Matumaini na matarajio katika maisha ya mwanadamu ndilo jambo linaloathiri na kuchochea zaidi harakati na mapambano yake maishani. Roho na msingi wa matarajio hayo ni kuwa na mtazamo mzuri kuhusiana na mustakbali wake ambao Mwenyezi Mungu amembashiria moja kwa moja kupitia Aya na Riwaya nyingi.

Serikali ya Imam Mahdi (ATF) inaarifishwa katika mtazamo mpya wa jamii iliyo bora zaidi kiuadilifu na kimaadili ambayo hadi leo haijawahi kushuhudiwa na mwanadamu yoyote. Kwa kudhihiri Imam Mahdi (ATF)tawala zote mbovu, dhalimu na fasidi zitafutwa kwenye uwanja wa historia. Ni wazi kuwa kufuta tawala kama hizo zinazotawaliwa na watawala fasidi, kunahitajia mapambano dhidi yao. Kuhusiana a suala hilo tunapasa kuzingatia nukta hii kwamba ili kufanikiwa katika lengo hilo, kunahitajika kuwepo serikali yenye nguvu na jeshi lililojizatiti vyema kwa silaha, serikali ambayo bila shaka itakuwa na maafisa na wafuasi walio na sifa maalum. Ni wazi kuwa maafisa na wafuasi kama hao wanapasa kuwa na uwezo mkubwa wa kuvumilia matatizo na machungu mengi yanayopatikana katika medani ya vita na kuongoza jamii katika mazingira magumu ya kudhihiri Imam Mahdi (ATF).Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu hajamlazimisha Imam wa Zama, Imam Mahdi (ATF) kubeba ujumbe huo peke yake na kwa msaada Wake wa mbinguni, bali jeshi kubwa la watu linapasa kushiriki katika tukio hilo muhimu la kihistoria ili nao wenyewe wapate kujibadilisha na kuwa na nafsi muhimu katika kuainisha mustakbali wao wa kihistoria.

Kulea wasaidizi wa Imam Mahdi

Kwa msingi huo, ni jambo la dharura sambamba na kuenea dhulma na uonevu duniani kulea watu wema na wanaofaa ili wamsaidie Imam katika majukumu na malengo yake ya kueneza uadilifu duniani. Hivyo basi, katika kipindi cha kabla ya kudhihiri Imam (ATF), wanaomsubiri mtukufu huyo wana jukumu kubwa na zito la kuwalea watu na jambii inayofaa ambayo itaweza kumsaidia Imam katika mapambano yake ya kurudisha uadilivu na usawa duniani. Jukumu la kwanza la wanaomsubiri Imam ni kuwa wanapasa kupata elimu na maarifa ya kutosha kuhusiana na Imam wao huyo wa Zama. Jambo hilo lina umuhimu mkubwa kadiri kwamba Mtume Mtukufu (SAW) amenukuliwa akisema katika Riwaya kwamba Mtu anayeaga dunia hali ya kuwa hamjui imam wa zama zake huwa amekufa kifo cha mtu jahili. Jukumu jingine ni kuwa wanapasa kujitenga na sifa zote mbaya na kujipamba kwa sifa bora na za kuvutia kidini. Naye Imam Swadiq (as) anasema: 'Kila mtu anayependa kuwa miongoni mwa wafuasi wa Mahdi Muahidiwa (ATF), anapasa kusubiri, kujitenga na maovu na kuwa na akhlaqi nzuri katika hali hiyo. Hivyo iwapo ataaga dunia katika hali hiyo.... atakuwa na malipo sawa na ya yule mtu aliyemdiriki (kumwona/kauishi katika zama za kudhihiri kwake) mtukufu huyo. Hivyo fanyeni juhudi na muendelee kusubiri.'

Wafuasi wa Imam wa Zama (ATF) mbali na kuwa wataalamu na watendaji wazuri kiuongozi, katika mtazamo wa kimaanawi pia ni watu bora na waliokamilika zaidi katika zama za Imam huyo. Viongozi wa kidini wamebainisha sifa za kimaanawi za wasaidizi na wafuasi wa Imam wa Zama (ATF) Elimu na maarifa, kumcha Mungu, kujiepusha na maovu, takwa, mwamko, ibada, dua, kifua kipana na udugu ni miongoni mwa sifa za wafausi wa Imam Mahdi (ATF).

Kwa hakika tunasubiri kudhihiri pambazuko lenye mvuto ambali ndiyo njia pekee itakayotutatulia matatizo yanayotukabili na hivyo kuwa mwanzo wa mambo yote mema na saada ya dunia na Akhera.

captcha