IQNA

Tizama Qiraa ya Qur'ani Tukufu ya Abdul Basit nchini Pakistan

12:44 - June 07, 2020
Habari ID: 3472845
TEHRAN (IQNA) – Qarii mashuhuri wa Qur'ani nchini Misri, Sheikh Abdul Basit Abdul Samad, ambaye aliaga dunia mwaka 1988, alikuwa maarufu kwa kusoma Qur'ani kwa sauti laini na aliwavutia wengi duniani.

Alisafiri katika nchi nyingi duniani kwa ajili ya kusoma Qur'ani Tukufu. Hapa chini ni qiraa yake ya Surah al-Waqia ya Qur'ani Tukufu akiwa nchini Pakistan.

Abdul Basit alizaliwa mwaka 1927 katika kijiji cha Almazaizah katika eneo la Armant kusini mwa Misri. Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad alikamilisha hifdhi ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 10 kijijini kwake kwa Ustadh Al Amir na akahitimu aina zote za kiraa ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 14.

Abdul Basit alipewa lakabu ya 'Koo ya Dhahabu' kutokana na kiraa yake ya kuvutia na alipendwa mno na wafuatiliaji wa masuala ya Qur'ani kwa kadiri kwamba hadi sasa anatambuliwa kuwa qarii mashuhuri na anayepesndwa zaidi wa Qur'ani.

Qiraa ya Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad iliwaathiri watu wengi na hata kuwavutia wasiokuwa Waislamu katika dini ya Kiislamu. Watu 6 waliingia katika dini ya Kiislamu baada ya kuathiriwa na kiraa yake mjini Los Angeles huko Marekani. Aidha inadokezwa kuwa nchini Uganda jumla ya watu 92 walisilimu katika majlisi ya kiraa ya msomaji huyo mashuhuri na watu wengine 72 pia walikubali dini tukufu ya Kiislamu katika majlisi nyingine baada ya kuvutiwa mno na usomaji wake.

Mwishoni mwa umri wake, Sheikh Abdul Basit alipatwa na maradhi ya kisukari na baadaye uvimbe wa ini. Alipelekwa London Uingereza kwa ajili ya matibabu baada ya kuzidiwa na maradhi na kurejeshwa Cairo wiki mbili baadaye. Inasemekana kwamba Sheikh Abdul Basit Abdus Samad alikuwa amehisi kwamba siku zake za kuishi duniani zinakaribia ukingoni na wakati wa kukutana na Mola Muumba ulikuwa unakaribia.

Qari huyo mashuhuri wa Misri aliaga dunia tarehe 30 Novemba mwaka 1988 katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

3903376

captcha