IQNA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
13:21 - July 10, 2020
Habari ID: 3472946
TEHRAN (IQNA) -Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, kusema urongo na kueneza chuki ni viungo muhimu katika sera za kigeni za Marekani.

Sayyid Abbas Mousavi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo  Alkhamisi ambapo amekanusha vikali tuhuma kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, Marekani inasema urongo.

Kauli hiyo ya Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ni jibu kwa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Mike Pompeo aliyedai kuwa Washington imekamata meli ya Iran iliyobeba silaha ikiwa njiani kuelekea Yemen.

Amesema lengo la maafisa wa serikali ya Washington kuibua madai yasiyo na msingi ni kuandaa mazingira ya kurefushwa vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya Iran ambavyo muda wake unamalizika tarehe 18 mwezi Oktoba, kwa mujibu wa Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria kuhusu mzingiro wa miaka mitano dhidi ya taifa la Yemen uliowekwa na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia na kubainisha kuwa, "Marekani imeamua kubuni madai ya urongo dhidi ya wengine, ili kukwepa kubeba dhima ya jinai zake na mienendo yake isiyo ya kibinadamu kwa kuiunga mkono Riyadh kwa hali na mali katika uvamizi wake dhidi ya Wayemen."

Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa maelfu ya raia waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani tokea Machi 2015.

3909601

Kishikizo: iran ، msemaji ، Abbas Mousavi ، Marekani ، Yemen ، Saudia
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: