IQNA

Rais Macron wa Ufaransa alaaniwa kwa msimamo wake wenye chuki dhidi ya Uislamu

21:15 - October 03, 2020
Habari ID: 3473226
TEHRAN (IQNA) - Waislamu wa Ufaransa wameudhika kwa kauli za chuki dhidi ya Uislamu zilizotolewa na rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron.

Yasser Louati, mwanaharakati wa Kiislamu ameandika katika ukurasa wake wa Twitter: Kukandamiza Waislamu limekuwa ni tishio, lakini sasa ni ahadi rasmi inayotekelezwa. Kwa mujibu wa mwanaharakati huyo wa Kiislamu, katika hotuba yake, Rais Emmanuel Macron amewapa ujasiri wa kuchukua hatua dhidi ya Waislamu wafuasi wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu mpaka.

Rim Sara Alaon, mwanaharakati wa asasi za kiraia  nchini Ufaransa, ameandika katika ukurasa wa kijamii wa Twitter: Macron anaeuelezea Uislamu kuwa ni dini ambayo leo iko kwenye hali ya mgogoro duniani kote.

Bruno Macaes ambaye ni mwandishi amesema: Macron hafichi tena hisia zake kuhusu Uislamu. Si suala tena la Uislamu wa misimamo mikali, bali sasa ni Uislamu wenyewe ndio tatizo.

Katika mwendelezo wa sera za kupiga vita Uislamu nchini Ufaransa, Emmanuel Macron jana alizindua mpango wa kulinda thamani za kisekulari za nchi hiyo dhidi ya kile kilichotajwa kama "Misimamo Mikali ya Kiislamu". Rais wa Ufaransa alidai kuwa Uislamu ni dini iliyo "kwenye mgogoro" ulimwengu mzima.

Katika hotuba yake hiyo ambayo imewaudhi Waislamu wa Ufaransa, Macron alisema, serikali yake itawasilisha muswada mwezi Desemba wa kuimarisha sheria ya 1905 ya nchi hiyo ambayo ilitenganisha rasmi Kanisa na utawala.

Mpango huo uliozinduliwa na Macron hapo jana unalenga pia kukabiliana na uwekezaji wa kigeni kwa ajili ya ujenzi wa misikiti na shule za kidini nchini humo pamoja na kukabiliana na maimamu wa misikiti wenye uraia wa kigeni.

Licha ya Ufaransa kuwa na idadi kubwa ya Waislamu miongoni mwa nchi za Ulaya lakini imeweka vizuizi vingi dhidi ya uhuru wa kuabudu kwa Waislamu wa nchi hiyo.

Uvaaji wa vazi la stara na heshima la Hijabu ni marufuku nchini Ufaransa kwa wanafunzi wa kike mashuleni na kwa watumishi wa umma katika maeneo yao ya kazi.

3472708

captcha