IQNA

Waislamu Ufaransa

Wanawake Waislamu sasa wahama Ufaransa kutokana na ubaguzi, chuki dhidi ya Uislamu

10:53 - February 18, 2024
Habari ID: 3478370
IQNA-Kuongezeka chuki katika ngazi za kisiasa na kijamii dhidi ya wanawake Waislamu hasa wanaovalia hijabu na niqabu nchini Ufaransa kumepelekea idadi kubwa ya wanawake hao waihame nchi hiyo ya Ulaya.

Shirika la habari la Anadolu limefanya mahojiano na wanawake 20 wa Kiislamu ambao wanasema ama wameondoka au wanapanga kuondoka nchini Ufaransa kutokana na kufanyiwa vitendo vya kibaguzi katika maeneo yao kazi kutokana imani na itikadi zao.

Ripoti ya Anadolu imesema kubaguliwa, kufanyiwa vitendo vya chuki kwa misingi ya dini na kutokubaliwa katika jamii ya Ufaransa kumewasukumu wanawake wengi wa Kiislamu kutafuta nafasi za ajira katika nchi nyingine.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mbali na kubaguliwa katika sehemu za kazi, wanawake Waislamu nchini Ufaransa wanakabiliwa pia na vitendo vya chuki na ubaguzi katika sekta za umma na elimu.

Nchini Ufaransa, ni marufuku kwenda shule na taasisi za serikali ukiwa na nembo za kidini, na kuvaa hijabu kumepigwa marufuku katika shule za umma tangu 2004. Mwaka 2010, sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na kujumuisha maeneo yote ya umma.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Marta Hurtado, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa alikosoa marufuku ya uvaaji hijabu kwa wanariadha wa Ufaransa katika Michezo ya Olimpiki, ambayo imepangwa kufanyika Paris mwaka huu.

Aidha Septemba mwaka uliopita, serikali ya Paris ilitangaza kupiga marufuku uvaaji wa abaya kwa wasichana katika shule za wasichana katika nchi hiyo ya Ulaya ambayo karibu asilimia 10 ya jamii yake imeundwa na Waislamu.

Serikali ya Ufaransa, inayoongozwa na Macron, imeshutumiwa kwa chuki dhidi ya Uislamu na mateso dhidi ya Waislamu kwa kisingizio cha kutokuwa na dini na kupinga ugaidi. Darmanin alisaidia kupitisha sheria ya 2021 ya "kupinga utengano", ambayo wanaharakati wanasema inalenga Waislamu na inaharamisha Uislamu katika mashirika ya kiraia. Mtazamo wa serikali ya Ufaransa umekosolewa kwa kukosa kuchochea misimamo mikali huku ikidai kupambana nayo.

3487224

Kishikizo: ufaransa waislamu macron
captcha