IQNA

Wanafunzi walaani Marufuku ya Hijabu Ufaransa, wasema ni 'Ubaguzi wa Rangi na Chuki Dhidi ya Uislamu'

19:20 - February 21, 2025
Habari ID: 3480247
IQNA-Chama cha Wanafunzi Waislamu wa Ufaransa (EMF) kimelaani vikali pendekezo la sheria inayopiga marufuku uvaaji wa Hijabu katika mashindano ya michezo, likiitaja kuwa "ya kibaguzi, ya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na ya ubaguzi wa kijinsia."

Katika chapisho lake kwenye X, kikundi hicho kilieleza kuwa sheria hiyo ni ya kibaguzi na inawazuia Waislamu kushiriki katika maeneo ya umma, hasa katika michezo. EMF ilisema kuwa pendekezo hilo linachochea ubaguzi kwa kisingizio cha kulinda uraia na utulivu wa umma. Chama hicho kimeonya kuwa "Sheria hii inawafanya Waislamu kuwa raia wa daraja la pili," na kusisitiza kuwa hatua kama hizi zinahujumu kanuni ya usawa.

Chama hicho cha wanafunzi pia kilikemea ukandamizaji wa taasisi za wanawake Waislamu huku kikihusisha marufuku hiyo inayopendekezwa na sheria ya mwaka 2004 ya Ufaransa inayozuia alama za kidini mashuleni, pamoja na marufuku ya mavazi ya abaya katika taasisi za elimu mwaka 2023.

Chama hicho kimesisitiza kuwa michezo, inayopaswa kuwa nyenzo ya kuunganisha jamii, sasa inageuzwa kuwa jukwaa la ubaguzi, na hivyo kimetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kuupinga mswada huo, ambao kimeutaja kuwa sehemu ya njama ya kuwakandamiza  Waislamu nchini Ufaransa.

Jumanne, Seneti ya Ufaransa iliendelea na mjadala wa mswada huo, ambao sasa utajadiliwa katika Bunge la Taifa, ambalo ni baraza la chini la bunge la nchi hiyo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International pia limekosoa muswada huo wa sheria na kusema: "Marufuku hii ni ya kibaguzi na inakiuka haki za binadamu. Wanawake wote wana haki ya kuchagua mavazi yao." Shirika hilo lilikosoa hatua hiyo likiitaja kuwa inatokana na chuki dhidi ya Uislamu na udhibiti wa mfumo dume juu ya mavazi ya wanawake Waislamu.

Pendekezo hili la hivi karibuni linakuja baada ya marufuku kadhaa tata nchini Ufaransa, ikiwa ni pamoja na marufuku ya mwaka 2023 ya abaya mashuleni.

3491953

Habari zinazohusiana
captcha