IQNA

Saudia yaruhusu Waislamu kutoka nje ya nchi kutekeleza ibada ya Umrah

15:38 - November 01, 2020
Habari ID: 3473317
TEHRAN (IQNA)- Serikali ya Saudi Arabia imewaruhusu waislamu wanaoishi nje ya ufalme huo kuingia nchini humo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra baada ya kufungwa mwezi Machi mwaka huu kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Televisheni rasmi ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, awamu ya tatu ya kuanza tena ibada ya Umra ilianza usiku wa Jumamosi ya jana na kwamba, mahujaji wa ndani na nje ya nchi wameruhusiwa kufanya ibada ya Umra, ziara na Swala ndani ya Msikiti wa Makka.

Awamu hiyo ya tatu inaruhusu kuanza hatua kwa hatua ibada ya Umra ya watu elfu 20, na watu elfu 60 kutekeleza ibada ya Swala kila siku ndani ya Masjidul Haram, sambamba na kulinda sheria za kukabiliana na virusi vya corona.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudia ilitangaza jana kwamba kundi la kwanza na Mahujaji kutoka nje ya Saudi Arabia litawasili nchini humo leo Jumapili.

Jumamosi ya jana pekee Saudi Arabia ilisajili kesi 402 za maambukizi ya virusi vya corona na 19 miongoni mwao waliaga dunia.

Hadi sasa watu 5,402 wameaga dunia nchini Saudi Arabia kutokana na virusi vya corona.

Utawala wa Saudia umekuwa ukikosolewa kwa kutozihusisha nchi za Kiislamu duniani katika maamuzi yake kuhusu ibada za Hija na Umrah. Hatua ya Saudia ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja pia imekosoelwa na maulamaa wa Kiislamu dunaini.

Msomi na mhadhiri wa chuo kikuu nchini Kuwait miezi michache iliyopita aliibua utata katika mitandao ya kijamii baada ya kusema hatua ya Saudia wa kupunguza idadi ya mahujaji mwaka huu itaubadilisha Msikiti Mtakatifu wa Makka, Al Masjid al Haram, kuwa sawa na jumba la makumbusho.

Hakim al-Mutairi mhadhiri wa Tafsiri ya Qur’ani Tukufu na Hadithi katika Chuo Kikuu cha Kuwait amekasirishwa na uamuzi wa Saudia wa kuwazuia mahujaji kutoka nje ya Saudia kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.  Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema: “Hii Hija itakuwa ni urasimu tu na Msikiti Mtakatifu wa Makka umebadilishwa kuwa jumba la makumbusho ambapo watakaohiji ni wale tu walioidhinishwa na utawala wa Saudia. Hii si Hija ambayo Mwenyezi Mungu SWT ameitaja katika aya ya 27 ya Suratul Hajj ifuatavyo: Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.”

3932505

Kishikizo: umrah saudia waislamu
captcha