Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imetangaza taratibu na miongozo mipya kama sehemu ya maandalizi ya Hija mwaka huu wa 1446 Hijria au 2025, zikiwa na lengo la kuhakikisha usalama na utulivu wa mahujaji katika kipindi hiki kitukufu.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, wizara hiyo ilieleza kuwa tarehe ya mwisho kwa waumini wa Umrah kuingia nchini humo itakuwa Jumapili, Aprili 13, 2025, huku tarehe ya mwisho ya kuondoka ikiwa ni Jumanne, Aprili 29, 2025.
Wizara ilionya kuwa kushindwa kuondoka kabla ya tarehe hiyo kutachukuliwa kama uvunjaji wa sheria.
Kuanzia Jumatano, Aprili 23, 2025, ufikiaji wa mji mtakatifu wa Makka utadhibitiwa vikali. Mtu yeyote atakayetaka kuingia Makka ni lazima awasilishe mojawapo ya nyaraka zifuatazo: kibali halali cha kazi, kitambulisho cha ukaazi kilichotolewa Makka, au kibali halali cha Hija.
Wakazi wa kigeni wanaoishi sehemu nyingine za Ufalme hawataruhusiwa kuingia Makka isipokuwa wawe na kibali maalum. Taarifa hiyo iliongeza kuwa wale watakaokiuka agizo hilo kwa kujaribu kuingia bila kibali watarudishwa kupitia kituo cha ukaguzi cha Al Shumaisi au vinginevyo.
Aidha, wizara ilitangaza kusitishwa kwa utoaji wa vibali vya Umrah kupitia jukwaa la “Nusuk” kuanzia Aprili 29 hadi Juni 10, 2025.
Zaidi ya hayo, watu wote wenye visa za aina nyingine isiyo visa rasmi ya Hija hawataruhusiwa kuingia au kuendelea kuwepo Makka kuanzia Aprili 29.
Miongozo hiyo pia inasisitiza kuwa raia wa kigeni wanaolazimika kuingia Makka au maeneo mengine matakatifu kwa madhumuni ya ajira wanapaswa kuomba vibali vya kusafiri kupitia mifumo rasmi inayohusika.
3492664