IQNA

Hatari ya kuzuka vita baina ya Ethiopia na Sudan

11:59 - January 14, 2021
Habari ID: 3473555
TEHRAN (IQNA) - Ndege a kivita za Ethiopia zilivuka mpaka na nchi jirani ya Sudan katika kile ambacho Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imekitaja kuwa ni taharuki hatari na isiyo na sababu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema hatua hiyo inaweza kuwa na matokeo hatari na kuibua taharuki zaidi katika eneo.

Nchi hizo mbili zimekuwa zikizozoana kwa miongo kadhaa kuhusu eneo la al-Fashqa ambalo liko katika mipaka ya kimataifa ya Sudan lakini ambalo limekuwa likikaliwa na wakulima wa Ethiopia. Mapigano mapya katika eneo hilo yameanza wiki mbili zilizopita.

Wakati huo huo, Ethiopia nayo imeituhumu Sudan kuwa imetuma idadi kubwa ya wanajeshi katika eneo hilo la mpakani linalozozaniwa na nchi mbili huku ikitahadharisha kuwa makabiliano ya kijeshi yanakaribia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia Dina Mufti ameashiria muelekeo wa nchi yake wa kutumia njia za amani kutatua mgogoro huo na kuonya kwamba ustahamilivu una mwisho wake.

Akizungumza Jumanne, Mufti amesema majeshi ya Sudan yanajipenyeza zaidi katika eneo linalozozoniwa na nchi hizo mbili la al-Fashqa.

Ameituhumu Sudan kuwa inachochea hali ya mambo huku akisema kuwa Ethiopia inafadhilisha udiplomasia kuliko vita lakini amesema kila kitu kina mwisho wake.

Waziri wa Habari wa Sudan na msemaji wa serikali Faisal Mohamed Saleh ameonya kuwa, nchi yake itajibu uvamizi wowote. Ameitaka Ethiopia kusitisha uhasama wake dhidi ya Sudan na wakulima Wasudan.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan inayatuhumu magenge ya Waethiopia kwa kushambulia eneo la al Fashqa Jumatatu ambapo wanawake watano na mtoto mmoja waliuawa.

Ethiopia inaituhumu Sudan kuwa inatumia fursa ya mgogoro wa Tigray kuchochea uhasama katika eneo la al-Fashqa. Kwa miezi kadhaa sasa jeshi la Ethiopia limekuwa vitani na waasi wa eneo la Tigray kaskaizni mwa nchi hiyo. Nchi hizo mbili aidha zinazozana kufuatia uamuzi wa Ethiopia kujenga bwawa kubwa katika Mto Nile. Misri na Sudan zimeungana kupinga ujenzi wa bwawa hilo linalojulikana kama An Nahda ambalo ni kubwa zaidi barani Afrika na ujenzi wake umegharimu dola bilioni tano.

3473700/

Kishikizo: sudan ethiopia misri
captcha