IQNA

Waislamu Ethiopia

Waislamu wa Ethiopia waandamana kupinga marufuku ya Hijabu katika baadhi ya shule

14:48 - January 23, 2025
Habari ID: 3480096
IQNA – Maelfu ya Waislamu walihudhuria maandamano mjini Mekelle, Ethiopia, siku ya Jumanne kupinga hatua ya shule za Axum kuwazuia wanafunzi wa kike wanaovaa Hijabu kuhudhuria masomo.

Shule katika eneo hilo zimekataa kufuata maamuzi ya mahakama na maagizo kutoka kwa Idara ya Elimu ya Kanda ya Tigray yanayoruhusu wanafunzi wa kike Waislamu kuvaa Hijabu darasani.

Maandamano hayo yaliyoandaliwa na Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Tigray, yaliendeshwa chini ya kaulimbiu “Atasoma Akiwa Amevaa Hijabu” na yaliwataka shule hizo siyo tu kutii maagizo bali pia kuheshimu tamaduni.

"Licha ya maamuzi wazi ya mahakama na maagizo kutoka idara ya elimu, binti zetu bado wanazuiwa kupata elimu. Hili linatia wasiwasi mkubwa katika eneo ambapo Uislamu ni sehemu ya tamaduni kwa karne nyingi," alisema Sheikh Adam Abdulkadir, Rais wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Tigray.

Maandamano hayo yanakuja baada ya wanafunzi Waislamu wa darasa la 12 kuzuiwa kusajiliwa kwa mitihani ya kitaifa huko Axum mapema mwezi huu kwa sababu ya kukataa kuvua hijabu zao.

"Hakuna sababu ya kisheria ya kuwalazimisha kuchagua kati ya imani zao za kidini na elimu yao. Wanayo haki ya kuhudhuria shule wakiwa wamevaa hijabu zao," alisema Mustefa Abdu, wakili aliyeshiriki maandamano hayo.

Kwa mujibu wa Kamil Abdu Oumer, mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Wollo, marufuku ya Hijabu pia inakiuka Kifungu cha 27 cha Katiba ya Ethiopia kinachoelekeza kuwa sheria zote za serikali zichapishwe katika Federal Negarit Gazeta.

Mahakama ya Wilaya ya Mji wa Axum hapo awali ilisimamisha agizo la kuzuia wanafunzi wa Kiislamu kuvaa Hijabu na kuitaka shule tano kujibu madai hayo. Hata hivyo, shule nyingi bado hazijatii.

"Hata Wakristo wanalaani marufuku hii, kwani kuvaa hijabu ni jukumu la kidini kwa wanawake Waislamu. Tunadai kwamba uamuzi huu uheshimiwe na binti zetu waruhusiwe kuendelea na masomo yao," alisema Abdurahman Billal mwenye umri wa miaka 65 aliyeshiriki maandamano hayo.

Hata hivyo, baadhi ya maafisa wa shule wameunga mkono marufuku hiyo.

"Shule si maeneo ya dini au siasa. Kwa hivyo, wanafunzi hawaruhusiwi kuingia shuleni wakiwa na alama au mavazi ya kidini," alisema Gebremeskel Gebregziabher, Naibu Mkurugenzi wa Shule ya Upili ya Axum, akiongeza kuwa sera hiyo imekuwepo kwa miaka mingi.

3491555

Kishikizo: ethiopia hijabu
captcha