IQNA

Hali ni tete Washington DC kabla ya kuapishwa Biden nchini Marekani

19:23 - January 17, 2021
Habari ID: 3473565
TEHRAN (IQNA)- Hofu imetanda kote Marekani wakati huu wa kukaribia kuapishwa Joe Biden kama rais wa nchi hiyo huku wanajeshi zaidi ya 30,000 wakiingia katika mji mkuu Washington DC kulinda usalama.

Siku ya Ijumaa, jeshi lilitangaza kuongeza wanajeshi 25,000 wakati wa kuapishwa kwa Biden, wengine 4,000 zaidi waliagizwa Alhamisi.

Ulinzi uko katika hali ya kiwango cha juu kuwahi kushuhudiwa kwa miaka mingi huku baadhi ya sehemu za mji wa Washington DC zimefungwa kabisa.

Maafisa wa usalama wa Marekani wanachukuwa tahadhari dhidi ya maandamano ya wafuasi wa rais anayeondoka Donald Trump katika miji mikuu ya majimbo yote 50 kipindi cha wikiendi.

Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI imetahadharisha idara za polisi juu ya kuwepo uwezekano wa waandamanaji wenye silaha nje ya majengo ya bunge katika majimbo yote 50 kuanzia Jumamosi hadi siku ya kuapishwa Rais mteule Joe Biden Januari 20, yaliochochewa na wafuasi wa Rais Donald Trump wanaoamini madai yake ya uongo ya wizi wa kura.

Waandamanaji nchini Marekani wanatarajiwa  kukusanyika nje ya majengo ya serikali kuunga mkono madai ya Trump ya kuibiwa kura kwenye uchaguzi uliopita huku vikosi vya usalama vikijiandaa kukabiliana na machafuko yanayotarajiwa kutokea nchini humo.

Zaidi ya majimbo kumi yameviweka tayari vikosi vya walinzi wa kitaifa kusaidia kuyalinda majengo ya bunge la Marekani, Capitol Hill kufuatia tahadhari kutoka kwa FBI la kitisho cha waandamanaji waliojihami kwa silaha. Wakati baadhi ya majimbo yakiwa yameweka uzio wa umeme ama vizuizi vingine ili kuimarisha usalama kwenye ikulu zao, Texas na Kentucky wamechukua hatua kali zaidi za kufunga kabisa eneo hilo na kuzuia watu kuingia. Kuimarishwa kwa ulinzi kote nchini humo kunafuatia shambulizi baya kabisa kwenye majengo ya bunge mjini Washington Januari 6 lililofanywa na wafuasi wa Trump na wenye misimamo mikali.

Wakati huo huo, FBI imemtia mbaroni mtu mmoja akiwa na silaha na risasi 500 haramu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Washington.

Mtandao wa habari wa Hill umewanukuu maafisa wa Marekani wakitangaza habari hiyo na kufafanua kwamba, mtu huyo ni kutoka jimbo la Virginia na amekamatwa katika kituo cha upekuzi akiwa na barua bandia ya mwaliko ya kushiriki katika sherehe za kuapishwa Joe Biden, silaha na zaidi ya risasi 500.

3948267

 

Kishikizo: trump biden marekani
captcha