IQNA

Bunge la Ufilipino laidhinisha ‘Siku ya Kitaifa ya Hijabu’

12:16 - January 27, 2021
Habari ID: 3473594
TEHRAN (IQNA) - Bunge la Ufilipino mnamo Januari 26, 2021, limepiga kura ya kuidhinisha Februari 1 kila mwaka kuwa ‘Siku ya Kitaifa ya Hijabu’.

Wajumbe 203 katika bunge hilo walipiga kura ya kuunga mkono  sheria hiyo ambapo hakuna mbunge yeyote aliyepinga mswada huo wala kujizuia kupiga kura.

Muswada huo ambao sasa ni sheria uliwasilishwa na wabunge Ansaruddin Abdul Malik Adiong na Amihida Sangcopan kwa lengo ka kuiwezesha jamii kuelewa zaidi sababu ya wanawake Waislamu kuvaa Hijabu.

Sheria hiyo pia inalenga kuwahimiza wasiokuwa Waislamu kuvaa Hijabu ili kuondoa dhana potovu iliyopo kuhusu vazi la Hijabu. Baadhi nchini Ufilipino wamekuwa wakilinasibisha vazi hilo na ukandamizaji  wa wanawake  au ugaidi.

Halikadhalika ‘Siku ya Kitaifa ya Hijabu Ufilipino’  inalenga kuwalinda wanawake Waislamu ili waweza kutekeleza maamurisho ya dini yao bila matatizo na kuwawezesha Wafilipino wote wafahamu kuwa Hijabu inalinda heshima ya mwanamke.

Idara za serikali, shule na sekta binafsi zitahimizwa zote kuadhimisha siku hiyo kila mwaka Februari  1.

Kwa mujibu wa takwimu kuna takribani Waislamu milioni 5.1 nchini Ufilipino ambao ni asilimia 6 ya watu wote nchini humo. Aghalabu ya Waislamu wanaishi katika baadhi ya maeneo ya Mindanao, na eneo la Moro.

3950004

captcha