IQNA

Katika Mahojiano na IQNA

Nazma Khan: Siku ya Hijabu Duniani ni Jukwaa la Kukuza Maelewano, Uvumilivu

19:38 - February 02, 2024
Habari ID: 3478289
IQNA - Siku ya Hijabu Duniani imekubaliwa duniani kote kama jukwaa la kukuza uelewano, uvumilivu, na mshikamano, mwanzilishi wa vuguvugu hilo alisema.

Kimataifa, inaonekana kama hatua nzuri kuelekea kuvunja imani potofu na kukuza ushirikishwaji," aliiambia Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) katika mahojiano.

Tarehe 1 Februari 2013 iliadhimishwa kama siku ya kwanza ya kila mwaka ya Hijabu Duniani (WHD). Siku hii ni ya kuwatambua mamilioni ya wanawake wa Kiislamu wanaochagua kuvaa hijabu na kuishi maisha ya staha.

Mwanzilishi wa vuguvugu hili ni mzaliwa  Bangladesh anayeishi Marekani, Nazma Khan, ambaye alikuja na wazo kama njia ya kukuza uhuru wa kibinafsi wa kujieleza kidini na uelewa wa kitamaduni kwa kuwaalika wanawake kutoka nyanja zote za maisha kuadhimisha hijabu kwa siku moja ambayo ni Februari 1 kila mwaka.

Kwa kuongeza ufahamu, Nazma anatarajia kukabiliana na baadhi ya utata kuhusu ni kwa nini wanawake wa Kiislamu wanachagua kuvaa hijabu.

Inakadiriwa kuwa watu katika zaidi ya nchi 150 hushiriki Siku ya Hijabu Ulimwenguni kila mwaka. WHD ina watu wengi wa kujitolea na mabalozi wa faharai duniani kote kuandaa matukio ya WHD ili kuleta ufahamu kuhusu hijab. Mabalozi hawa wanatoka nyanja mbalimbali. Kwa kuongezea, WHD imeidhinishwa na watu wengi mashuhuri duniani wakiwemo wasomi, wanasiasa, na watu mashuhuri duniani kote.

Kulikuwa na matukio mengi tangu kuanzishwa kwa Siku ya Hijabu Duniani. Mojawapo yao imekuwa kutambuliwa kwa siku hiyo na Jimbo la New York tangu 2017.

Katika mahojiano na IQNA, alikumbuka uzoefu wake kama mgumu.

“Naitwa Nazma Khan. Mimi ni mtoto wa 3 kati ya ndugu zetu wanne. Tulihamia NYC kutoka Bangladesh katikati ya miaka ya 1990. Nina shahada ya kwanza katika Biolojia. Pia nimesomea Biomedical Engineering. Sasa, nimeolewa na nimebarikiwa na watoto wawili wazuri. Alhamdullilah!” aliiambia IQNA.

“Nikiwa Bronx, New York City, nilikumbana na ubaguzi mkubwa kutokana na hijabu yangu. Katika shule ya sekondari, walizoea kuniita ‘Batman’ au ‘ninja.’ Nilipoingia chuo kikuu, mashambulizi ya 9/11 yalitokea. Sasa, niliitwa Osama bin laden au gaidi. Hali ilikuwa mbaya sana na hivyo nilianzisha kampenia ya uhamasishaji.

"Lengo langu kuu la kuzindua Siku ya Hijabu Duniani ni kuelimisha na kuleta ufahamu wa Hijabu duniani kote ili dada zangu waweze kuvaa hijabu bila kukabiliwa na ubaguzi na chuki," alisema.

Kulingana na Nazma Khan, "Siku ya Hijabu Duniani imekubaliwa ulimwenguni kote kama jukwaa la kukuza uelewano, uvumilivu na mshikamano. Nchini Marekani, inatambulika kwa kukuza tofauti za kitamaduni na uhuru wa kidini, kuhimiza mazungumzo kuhusu umuhimu wa hijabu. Kimataifa, inaonekana kama hatua chanya kuelekea kuvunja imani potofu na kukuza ushirikishwaji.

Alipoulizwa kuhusu changamoto kuu zinazowakabili wanawake wanaovaa hijab nchini Marekani, alisema, “Hijabi (wanaovaa Hijabu) nchini Marekani wanakabiliwa na changamoto kama vile mitazamo potofu kuhusu imani yao, imani potofu za kitamaduni, ubaguzi wa mara kwa mara, na hitaji la kuongeza uelewa kuhusu chaguo la kuvaa hijabu. Zaidi ya hayo, kuleta mlingano baina ya itikadi za kidini na matazamio ya jamii kunaweza kuwa changamoto.”

Mwanzilishi wa Siku ya Hijabu Duniani amesema chuki dhidi ya Uislamu ay Islamophobia ni matokeo ya ujinga. "Ninaamini sababu ya msingi ya chuki dhidi ya Uislamu ni ujinga na ukosefu wa elimu sahihi kuhusu Uislamu. Ninalaumu sana vyombo vya habari na watu walio madarakani kwa kueneza habari potofu kuhusu Uislamu.”

Kwa habari zaidi kuhusu matukio na shughuli maalum kwenye Siku ya Hijabu Duniani, angalia www.worldhijabday.com

 

captcha