IQNA

Maombolezo

Mjumuiko mkubwa mjini Najaf katika kumbukizi ya kuuawa shahidi Imam Ali AS

13:21 - April 01, 2024
Habari ID: 3478611
IQNA - Zaidi ya waumini milioni moja walikusanyika kwenye HaramTukufu ya Imam Ali (AS) huko Najaf, Iraq katika maombolezo yaliyofanyika wakati wa kumbukumbu  ya kifo chake cha kishahidi na kushika sambamba na ibada za Usiku wa Laylatul Qadr.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iraq, hafla hiyo ilihudhuriwa pia na makumi ya maelfu ya waumini waliosafiri kuelekea mji huo wa Iraq kutoka mataifa mengine.

Wasimamizi wa Haram hiyo takatifu walitangaza kwamba zaidi ya mita za mraba 18,000 za nafasi inayozunguka eneo hilo la ibada zimetengwa ili kuwakaribisha wafanyaziara, kuandaa milo ya futari na kutenga maeneo ya kupumzika.

Zaidi ya hayo, nyumba ya wageni ya Haram Tukufu ya Imam Ali AS  ilitoa milo zaidi ya 100,000 kwa wafanyaziara wakati wa futari katika uwanja wa Bibi Fatima SA.

Imam Ali (AS), Imam wa kwanza wa Waislamu wa Shia, aliuawa shahidi katika siku ya 21 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani zaidi ya karne kumi na tatu zilizopita. Tukio hili huadhimishwa kila mwaka na Waislamu wa madhehebu ya Shia na wengine duniani kote.

Katika mkesha wa kumbukumbu ya kifo cha kishahidi cha Imam Ali AS, ibada za maombolezo hufanyika kwenye kaburi lake tukufu huko Najaf, Iraq. Kaburi hilo tukufu limepambwa kwa bendera iliyoandikwa “Fuzt Wa Rabb al-Kaaba”, maneno yaliyosemwa na Imam Ali AS alipopigwa kichwani. Maana yake ni “Naapa kwa Mola wa Al-Kaaba kwamba nimefuzu”.

Siku mbili kabla ya kifo chake, Imam Ali bin Abi Twalib alipigwa upanga kichwani na mmoja wa wafuasi wa kundi la Khawarij wakati alipokuwa katika sijda ya Swala akimwabudu Mwenyezi Mungu msikitini. Siku kama ya leo Imam Ali AS aliaga dunia kutokana na majeraha makubwa aliyopata na hivyo kufikia matarajio yake makubwa ambayo alikuwa akiyatamani daima, yaani kuuliwa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu SW.

Kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib (as) kulikuwa msiba mkubwa na usioweza kufidika kwa Uislamu na Waislamu.   

3487759

captcha