IQNA

Mufti wa Uganda asema amejiuzulu kuulinda Uislamu

11:24 - April 06, 2021
Habari ID: 3473787
TEHRAN (IQNA) Mufti Mkuu wa Uganda anayefungamana na mrengo wa 'Kibuli Hill' mjini Kampala, Sheikh Silman Kasule Ndirangwa alitangaza kujiuzuli wadhifa huo Alhamisi iliyopita.

Sheikh Ndirangwa alichukua wadhifa huo Aprili 2015 kufuatia kifo cha aliyekuwa akishikilia cheo hicho, Sheikh Zubair Kayongo.

Sheikh Ndirangya alikuwa wa pili kushika wadhifa wa Mufti Mkuu wa Waislamu wa Uganda wanaofuata mrengo wa 'Kibuli Hii' ambao uliibuka mwaka 2009 baada ya kujitenga na uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Uganda (UMSC) wenye makao yake eneo la Old Kampala. Mgawanyiko huo wa Waislamu Uganda uliibuka kufuatia tuhuma za utumizi mbaya wa mali za Waislamu.

Mrengo huo wa Kibuli Hill nao pia umekuwa na hitilafu za ndani baada ya mmoja wa viongozi wake mashuhuri, Sheikh Obed Kamulegeya, ambaye alikuwa mstari wa mbele kujitenga na ule mrengo wa Old Kampala, naye pia kutangaza kujitenga wenzake wa mrengo wa Kibuli Hill.

Haijabainika sababu kamili za kujiuzulu Sheikh Nirangwa lakini taarifa yake ya kujiuzulu iliashiria uwezekano wa kuwepo hitilafu katika mrengo huo. Katika barua yake hiyo, Sheikh Ndirangwa alisema: "Napenda kuwajulisha ndugu na dada zangu kuwa, kuanzia leo najiuzulu kama kiongozi wa Waislamu. Nimechukua uamuzi huu kwa maslahi ya Uislamu na kwa ajili ya kuulinda na kuuhami Uislamu kwani mini ni mfuasi mdogo wa Uislamu. Uislamu ni dini  kubwa. Kwa kuuheshimu Uislamu siwezi kuzozoana na wakubwa wangu...hii ndio sababu imepelekea nijiuzulu."

Amesema kujiuzulu kwake kutawawezesha wengine wachukua hatamu za uongozi kwa maslahi ya Uislamu.

Mrengo wa Kibuli Hill uko chini ya ushawishi wa Prince Kassim Nakibinge, ambaye ni mjukuu wa Nuhu Mbogo, anayetajwa kuwa 'babu wa Uislamu' Uganda.

Naibu Mufti mkuu wa mrengo huo Sheikh Mahmood Kibaate amesema ameshangazwa na hatua ya kujiuzulu Mufti Mkuu.

Katika barua ya ke ya kujiuzulu Sheikh Ndirangwa pia alimshukuru Rais Yoweri Museveni kwa msaada wake kwa Waislamu wa Uganda ambapo ameashiria hatua ya rais kuwapa zawadi ya magari Makadhi wa wilaya zote za Uganda.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, zawadi hizo za Museveni ziliibua mgawanyiko katika mrengo wa Kibuli Hill huku baadhi ya viongozi waandamizi wakitaka zawadi hizo zirejeshwe.

3962717

Kishikizo: uganda waislamu mufti
captcha