IQNA

Hamas: Wapalestina wajitokeze kwa wingi wakati wa kumbukumbu kuteketezwa moto Msikiti wa Al Aqsa

13:04 - August 20, 2021
Habari ID: 3474210
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetoa mwito kwa Wapalestina kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya kukumbuka tukio chungu la kuteketezwa moto msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel.

Taarifa iliyotolewa na Hamas kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa 51 tangu msikiti wa Al Aqsa ulipochomwa moto imeeleza kwamba, msikiti huo ni mstari mwekundu kwa Wapalestina na ikawataka wananchi hao washiriki kwa wingi katika maandamano ya kukumbuka tukio la kuchomwa moto mahali hapo patakatifu.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: "Taifa letu litakata mikono ya watu wanaotaka kuuvunjia heshima msikiti wa Al Aqsa".

Harakati ya Hamas imeashiria pia kutiwa nguvuni na kuwekwa mbali na msikiti wa Al Aqsa Sheikh Raid Salah, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Palestina katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la Israel, na kueleza kwamba hatua hiyo ni njama iliyofanywa na adui Mzayuni ili kupadhibiti mahala hapo patakatifu.

Siku ya Jumanne wiki hii, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulirefusha kwa muda wa miezi mingine sita kifungo cha fargha ilichomhukumu Sheikh Raid Salah, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Palestina katika ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1948 na kupewa jina la Israel.

Tarehe 21 Agosti mwaka 1969, Msikiti mtukufu wa Al Aqsa, ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na moja ya maeneo matakatifu yanayoheshimiwa na wafuasi wa kweli wa dini za mbinguni ulichomwa moto na kuharibiwa na Wazayuni.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mhalifu huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).

3991881

captcha