IQNA

Kiongozi wa Ansarullah

Saudia inashirikiana na Israel, Marekani katika njama dhidi ya Waislamu

12:59 - September 03, 2021
Habari ID: 3474252
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema Saudi Arabia, utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani ziko kwenye muungano mmoja.

Sayyid Abdul-Malik Badruddin Al-Houthi ameeleza kwamba dhulma ya Marekani na utawala wa Kizayuni ni tishio kwa dini, amani, uhuru na heshima ya umma wa Kiislamu.

Al-Houthi ameongeza kuwa, msimamo wa taifa la Yemen dhidi ya dhulma ya Marekani na utawala wa Kizayuni ni msimamo wa haki; na watu wanaojiunga na muungano wa Marekani na utawala huo haramu wanakosea.

Katibu Mkuu wa Ansarullah ya Yemen amesema, uchokozi na uvamizi iliofanyiwa Yemen na njama inayotekelezwa dhidi ya nchi za eneo vinainufaisha Marekani na Israel na akasisitiza kuwa, haiwezekani kuunyamazia kimya utumiaji mabavu wa Marekani na utawala wa Kizayuni, wakati tawala hizo mbili zinaufanyia dhulma umma mzima wa Kiislamu kuanzia Yemen hadi Palestina.

Sayyid Abdul-Malik Badruddin Al-Houthi amebainisha pia: "kama tungezembea katika vita, vituo vya kijeshi vya Marekani, Uingereza na Israel vingekuwepo Sana'a na mikoa mingine ya Yemen, lakini kwa kuendelea kukabiliana na adui, karibuni hivi tutayakomboa maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu na muungano vamizi wa Saudia.

Jana Alkhamisi, wananchi wa Yemen walifanya maandamano makubwa katika mkoa wa Sa'da kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyokufa shahidi Zaid Ibn Ali AS na kutoa nara na kaulimbiu dhidi ya Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

/3475612

captcha