IQNA

Kiongozi wa Ansarullah akosoa Saudia kwa kuwazuia Waislamu kutekeleza Ibada ya Hija

12:27 - August 10, 2021
Habari ID: 3474176
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza kuwa hatua ya utawala wa Aal Saud ya kuzuia kufanyika ibada tukufu ya Hija kwa mwaka wa pili mfululizo kwa kisingizio cha corona ni kuivunjia heshima Nyumba Tukufu ya Allah.

Akihutubia kwa mnasaba wa kuingia mwaka mpya wa Hijria wa 1443, Sayyid Abdulmalik Badruddin Al Houthi amesema, Hija ambayo ni nembo mojawapo ya Kiislamu ni nembo ya ulimwengu na kimataifa pia, hivyo kuiwekea mpaka, si tu kunaathiri heshima ya nguzo hiyo ya Kiislamu, lakini pia ni hatua hatari dhidi ya Ulimwengu wa Kiislamu.

Sayyid Abdulmalik Al Houthi ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa Ansarullah kisingizio kilichotumiwa na Saudia kuzuia kufanyika ibada ya Hija hakikubaliki na si cha kisheria kwa hivyo harakati hiyo inautaka utawala huo usizuie kufanyika Hija; na nchi za Kiislamu pia ziushinikize utawala wa Aal Saud uandae mazingira ya kuziwezesha nchi zingine kutekeleza ibada ya Hija.

Duru za habari zilitangaza jana Jumatatu kuwa, serikali ya Saudi Arabia imewanyima raia wa nchi 33 zikiwemo Iran na Uturuki kwenda kutekeleza Hija ndogo ya Umra.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Abdulmalik Al Houthi amezungumzia pia mapambano ya wanamuqawama wa Palestina yaliyopewa jina la "Upanga wa Quds" na akasema, mapambano hayo yamezifedhehesha nchi zilizoanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitizia pia jukumu walilonalo Waislamu wote la kuunga mkono suala la Palestina na akaeleza kwamba, hatua ya utawala wa Saudia ya kutoa hukumu za vifungo vya hadi miaka 22 jela kwa Wapalestina iliowakamata ni sawa na kushirikiana na adui Mzayuni; na endapo utawala wa Aal Saud utakuwa bega kwa bega na muqawama wa Palestina, Ansarullah itaunga mkono msimamo huo.

3989592

captcha