IQNA

Hizbullah yatangaza azma ya kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Lebanon

19:44 - October 06, 2021
Habari ID: 3474387
TEHRAN (IQNA)- Afisa wa ngazi ya juu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kundi hilo la muqawama lina haki ya kutumia njia zote halali kulilinda taifa la Lebanon, na kuvunja vikwazo na mzingiro wa Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Sheikh Naim Qassem, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema hayo katika mkutano wa wanazuoni wa Kiislamu mjini Beirut na kuongeza kuwa, "Tuna kila haki ya kutumia njia zozote halali kisheria ambazo zitaleta matokeo chanya, huku tukipigania uhuru na ukombozi wa taifa letu."

Sheikh Qassem ameeleza bayana kuwa, harakati ya Hizbullah katu haitakubali kufuata dikrii na amri ya mabeberu zenye lengo la kufanikisha njama za utawala haramu wa Israel katika eneo la Asia Magharibi, na pia haitaruhusu kuhujumiwa uhuru wa nchi hiyo wakati huu inapokabiliana na ukaliaji wa mabavu wa ardhi yake.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, harakati hiyo ya Kiislamu haitakubali uhasama na uadui wa yeyote yule upite hivi hivi bila kupewa jibu mwafaka.

Amefafanua kwa kusema: Lazima tusimame kidete na tuwe tayari kujibu chokochoko za maadui katika ngazi ya kijeshi, kitamaduni, kiuchumi, kijamii na kiakhlaqi. 

Sheikh Naim Qassem, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon sanjari na kupongeza hatua ya kuundwa serikali mpya nchini Lebanon iliyohitimisha mkwamo wa kisiasa wa miezi 13 amesema kuwa, hatua hiyo pamoja na kuwasili mafuta ya Iran nchini humo ni mafanikio mawili makubwa si tu kwa Walebanon, lakini pia kwa mrengo wa muqawama. 

4002732

captcha