IQNA

Maulid ya Mtume Muhammad SAW yawavutia mamilioni nchini Yemen

11:19 - October 19, 2021
Habari ID: 3474440
TEHRAN (IQNA)- Mamilioni ya watu wa Yemen wamejitokeza katika Maulidi ya Mtume Muhammad SAW y katika miji mbalimbali ya Yemen ukiwemo mji mkuu Sanaʽa.

Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Masirah, Waislamu wa mikoa mingine 14 nao wamejitokeza kwa wingi mkubwa katika kuonesha haiba na nguvu za wapenzi wa Mtume Muhammad SAW kwenye Maulidi hayo.

Mamilioni ya Waislamu wameshiriki kwa shauku na hamasa kubwa katika maadhimisho hayo ambayo kwa mujibu wa baadhi ya hadithi zilizopokewa na Waislamu wa Kisuni, Mtume Muhammad SAW alizaliwa mwezi 12 Mfunguo Sita. Mwezi 12 Mfunguo Sita pia ndio siku kinapoanza kipindi cha Wiki ya Umoja kati ya Waislamu.

Kwa vile kuna kauli tofauti kuhusu siku ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW, huku tarehe maarufu zaidi kwa upande wa Waislamu wa Kisuni ni mwezi 12 Mfunguo Sita na kwa upande wa Waislamu wa Kishia tarehe maarufu zaidi ya kuzaliwa Mtume ni mwezi 17 Mfunguo Sita, Imam Khomeini MA alikitangaza kipindi cha baina ya tarehe hizo mbili kuwa Wiki ya Umoja ili Waislamu waweze kukitumia vizuri kuimarisha umoja na mshikamano baina yao na si kugombana kwa tofauti hiyo ndogo.

Kamati iliyosimamia Maulidi ya Mtume huko Yemen imesema kuwa, Waislamu wanawake wametenganishwa na wanaume kwenye sherehe hizo huku wanawake wakitengenewa maeneo yao maalumu ya kuadhimisha Maulidi ya Mtume SAW bila ya kuchanganyika na wanaume. Abdul Malik Badruddin al Houthi, Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amehutubia Waislamu na kusisitiza kuwa, mapenzi yao makubwa kwa Mtume ndiyo yanayowafanya wananchi wa Yemen wawe imara zaidi.

4006151/

captcha