IQNA

Mpalestina akataa dola milioni tano alizopewa na Wazayuni ili aihame nyumba yake

17:58 - December 10, 2021
Habari ID: 3474661
TEHRAN (IQNA)- Mpalestina amekataa dola milioni tano za Kimarekani kutoka wa Wazayuni ambao walikuwa wanataka kumiliki nyumba yake katika mtaa wa Sheikh Jarrah mjini Quds (Jerusalem).

Abdel-Fattah Eskafi ni mmoja kati ya Wapalestina ambao wanakabiliwa na hatari ya nyumba zao kunyakuliwa kwa nguvu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akizungumza na shirika la habari la AA, amesema kati hatasalimu amri mbele ya matakwa ya walowezi wa Kizayuni.

“Familia yangu ilifurushwa tokea mwaka 1948 (wakati utawala bandia wa Israel ulipoanzishwa). Tulikuwa tunaishi Baqa’a nje ya Quds Magharibi na kisha tukahamia Quds Mashariki. Hivi sasa naishi katika nyumba yenye ukubwa wa mita 130 na familia yangu ya watu 14 wakiwemo watoto na wajukuu.”

Anasema nyumba yao ya zamani bado iko Baqa’a lakini sasa ni walowezi wa Kizayuni wanaoishi hapo.  Ameongeza kuwa Wazayuni walinyakua nyumba hiyo kwa kutumia nyaraka ghushi na kuisajili kwa jina lao.

Hivi karibuni askari hao walivamia na kubomoa kiholela makazi ya Wapalestina katika mtaa wa Sheikh Jarrah katika mji mtakatifu wa Quds.

 Eneo hilo ambalo lilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1967 lina zaidi ya Wapalestina 3000 na linachukuliwa kuwa mstari wa mbele wa kutetea Msikiti wa al-Aqsa. Kwa maneno mengine ni kwamba mtaa huo uko kwenye kitovu cha mji wa Quds na unayaunganisha maeneo ya mashariki na magharibi mwa mji huo.

Ni kutokana na umuhimu wa kijografia wa eneo hilo ndipo utawala wa Israel ukawa unatekeleza kila njama, zikiwemo za kujenga vitongoji vya Mayahudi, kubomoa nyumba za Wapalestina, kuwaua kigaidi na kubomoa nyumba zao, ili kuwafukuza katika eneo hilo na kulifanya kuwa la walowezi wa Kiyahudi.

Kwa madhumuni ya kufikia lengo hilo, utawala huo tayari umefukuza makumi ya familia za Wapalestina katika mtaa huo na kutishia kufukuza wengine wengi katika siku zijazo. Kuhusu ukandamizaji huo dhidi ya Wapalestina, Mohammad Shtayyeh, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kwamba matukio ya Quds na Sheikh Jarrah, ni mfano mpya wa siasa zinazotekelezwa kimfumo kwa ajili ya kuwafanya Wapalestina kuwa wakimbizi.

3476874

captcha