IQNA

Serikali ya Ufaransa yavunja 'Baraza la Fiqhi la Waislamu'

16:32 - January 11, 2022
Habari ID: 3474793
TEHRAN (IQNA)-Serikali ya Ufaransa imevunja Baraza la Fiqhi la Waislamu wa Ufaransa (CFCM) ikiwa ni muendelezo wa sera zake za kuwakandamiza Waislamu.

Baraza hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2003 na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wakati huo Nicholas Sarkozy limekuwa likitumiwa kama chombo cha mawasiliano baina ya serikali na Waislamu.

Kwa mujibu wa taarifa taasisi mpya inayojulikana kama 'Jukwall la Uislamu Ufaransa' inatazamiwa kuchukua nafasi ya baraza hilo.

Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni muendelezo wa sera zilizoanzishwa na serikali ya Ufaransa mwaka jana kukabiliana na kilekinachosemekana kuwa ni 'misimamo mikali ya kidini'

Aliyekuwa mwenyekiti wa CFCM Mohamed Mousavi  bado haijulikani iwapo jumuiya za Waislamu Ufaransa zitaafiki kushirikiana na taasisi mpya iliyobuniwa na serikali.

Viongozi wa Kiislamu Ufaransa wanapanga kukutana hivi karibuni kujadili mafunzo mapya kwa Maimamu na pia kuainisha mbinu za kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu.

Hivi karibuni  kamati maalumu ya Bunge la Kitaifa la Ufaransa iliidhinisha sheria ya 'thamani za jamhuri' ambazo zilipendekezwa na rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokitaja ni 'Uislamu wa wanaotaka kujitenga.'

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin amedai katika ukurasa wake wa Twitter kuwa sheria hiyo inalenga kulinda thamani za jamhuri sasa na siku za usoni.

Katika miezi ya hivi karibuni Ufaransa imeshadidisha mbinyo dhidi ya Waislamu nchini humo ambapo hata maduka ya Waislamu yanafungwa kwa visingizio mbali mbali.

Maafisa wa serikali za mitaa Ufaransa sasa wanatumia kila kisingizio kufunga biashara za Waislamu ikiwa ni katika kutekeleza sera jumla za Rais Emmanuel Macron ambaye ameanzimia kuwadhoofisha Waislamu nchini humo.

Ufaransa ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016, kuna zaidi ya Waislamu milioni 5.7 Ufaransa ambao ni takribani asilimia 8.8 ya watu wote nchini humo.

4027814

captcha