IQNA

TI Pakistan: Kufunga misikiti Ufaransa ni chuki dhidi ya Uislamu

23:12 - January 15, 2022
Habari ID: 3474809
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa Jumuiya ya Tanzim Islami (TI) ya Pakistan amelaani vikali hatua ya Ufaransa kufunga msikiti katika mji wa Cannes nchini humo.

Shujauddin Sheikh ameitaja hatua hiyo ya Ufaransa kuwa aina mbya ya ugaidi wa wenye chuki dhidi ya Uislamu.

Akizungumza Ijumaa, amesema kufungwa msikiti mwingine Ufaransa kwa mara nyingine kumewathibitishia walimwengu kuwa, nchi za Magharibi zimeishiwa kimaadili na hazina uwezo wa kustahamili kuona Waislamu waliowachache wakitekeleza ibada zao.

Kiongozi huyo wa Kiislamu Pakistan amesema nchi za Magharibi kama Ufaransa zinadai kutetea demokrasia, usawa na uhuru wa kuabudu lakini zimekuwa zikiunga mkono kuvunjiwa heshima Uislamu sambamba na kuwazuia Waislamu kutekeleza ibada zao.

Hivi karibuni Ufaransa iliendeleza ukandamizaji wake wa Waislamu kwa kutangaza kufunga msikiti mmoja katika mji wa Cannes.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin ametangaza Jumatano kuwa, msikiti huo uliop katika mji wa Cannes ulio katika pwani pwani ya Bahari ya Mediterranean kusini mashariki mwa Ufaransa. Darmanin amedai kuwa wahubiri katika msikiti huo wametoa matamshi dhidi ya Mayahudi na kuunga mkono makundi yanayodaiwa kuwa na misimamo mikali ya kidini ambayo ni CCIF na BarakaCity.

Katika miezi ya hivi karibuni Ufaransa imeshadidisha mbinyo dhidi ya Waislamu nchini humo ambapo hata maduka ya Waislamu yanafungwa kwa visingizio mbali mbali.

Maafisa wa serikali za mitaa Ufaransa sasa wanatumia kila kisingizio kufunga biashara za Waislamu ikiwa ni katika kutekeleza sera jumla za Rais Emmanuel Macron ambaye ameanzimia kuwadhoofisha Waislamu nchini humo.

Ufaransa ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016, kuna zaidi ya Waislamu milioni 5.7 Ufaransa ambao ni takribani asilimia 8.8 ya watu wote nchini humo.

3477373

captcha