IQNA

Makaburi ya Waislamu Ufaransa yahujumiwa

20:36 - December 14, 2021
Habari ID: 3474673
TEHRAN (IQNA)- Makaburi ya Waislamu katika mji wa Mulhouse, mashariki mwa Ufaransa yamehujumiwa na watu wasiojulikana Jumapili jioni.

Jamii ya Waislamu Ufaransa imeshtushwa tena na kitendo kingine cha chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia ambapo watu wenye chuki wamevamia na kuvunjia heshima makaburi ya Waislamu mjini Mulhouse katika eneo la Haut-Rhin mashariki mwa Ufaransa.

Meya ya Mulhouse Michele Lutz amelaani vikali kitendo hicho na kusema  makaburi ni nembo inayopaswa kuheshimiwa. "Nafahamu familia zimeshtusjwa na kile zilichokiona. Makaburi yanapaswa kubakia kuwa eneo tulivu na la kutafakari," ameongeza.

Mbunge wa Haut-Rhin, Bruno Fuchs wa chama cha Democratic Movement ametangaza kushikamana na Waislamu huku akilaani kitendo hicho. Aidha amewataka Waislamu wawasilishe rasmi malalamiko yao kwa Idara ya Polisi.

Kufuatia kitendo hicho, Baraza kuu la Waislamu Ufaransa limelaani vikali kuvunjiwa heshima makaburi ya Waislamu na kutaka polisi wachukue hatua za kuwakamata wahusika wa jinai hiyo.

Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa wimbi jipya la vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu ambapo misikiti imekuwa ikilengwa. Mwezi Novemba misikiti milwili mjini Besencon ilihujumiwa na watu waliochora misalaba katika kuta za misikiti.

Aidha fufanya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kuwa jambo la kawaida sasa ni sera ya wanasiasa kote Ufaransa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa sasa imezindua laini maalumu ya simu ambapo imewataka raia kuripoti 'misimamo mikali ya Kiislamu.' Kimsingi ni kuwa hivi sasa kila Muislamu  Ufaransa anatazamwa kama mshukiwa wa uhalifu.

Bunge la Ufaransa pia limepitisha   sheria ya 'thamani za jamhuri' ambazo zilipendekezwa na rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokitaja ni 'Uislamu wa wanaotaka kujitenga.'

Kwa kuzingatia kuwa uchaguzi wa Ufaransa utafanyika Aprili 2021, wanasiasa nchini humo wanajaribu kuvutia kura za wapiga kura wa mrengo wa kulia kwa kueneza chuki dhidi ya Uislamu. Kwa msingi huo hali ya Waislamu inatazamiwa kuwa mbaya zaidi wakati huu wa kkukaribia uchaguzi mkuu nchini humo.

Ufaransa ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016, kuna zaidi ya Waislamu milioni 5.7 Ufaransa ambao ni takribani asilimia 8.8 ya watu wote nchini humo.

captcha