IQNA

OIC yalaani hujuma ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al Aqsa

19:46 - April 15, 2022
Habari ID: 3475129
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani hujuma iliyofanywa na walowezi wa Kizayuni wakisaidiwa na askari wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa.

Mapema leo (Ijumaa), wanajeshi wa Israel wakishirikiana na walowezi wa Kizayuni wameshambulia tena Msikiti wa Al-Aqsa na kuwajeruhi Wapalestina wasiopungua 150. Wapalestina wengine 400 wametiwa nguvuni.

Harakati ya Hamas ilikuwa imetoa wito kwa makundi mbalimbali ya wanamapambano wa Kipalestina kuelekea Quds na Msikiti wa al Aqsa tangu alfajiri ya leo kwa ajili ya kuyalinda maeneo hayo mawili matakatifu dhidi ya hatari ya wavamizi na mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu leo Ijumaa imeonya katika taarifa yake kuhusu vitisho vya makundi yenye misimamo mikali ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na Msikiti wa Al-Aqsa.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, Hussein Ibrahim Taha ameulaumu utawala wa Kizayuni kwa madhara yanayoweza kujitokeza ya kuendeleza mauaji ya kinyama dhidi ya wananchi wa Palestina, na vilevile kwa kuendelea kuvunjia heshima maeneo matakatifu, jambo ambalo linachochea migogoro ya kidini, misimamo mikali na ukosefu wa amani katika eneo hilo. 

Katika upande mwingine Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameitaka jamii ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la umoja huo kuilaani Israel kwa mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina na hatua zake za mara kwa mara za kuyavunjia heshima maeneo matakatifu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Kwa mujibu wa tovuti ya Kipalestina ya Felestin Al Youm, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Israel katika siku 15 zilizopota katika Ukingo wa Magharibi imefika 17.

4049613

 

captcha