IQNA

Uchambuzi

Nukta kadhaa kuhusu hujuma ya Wazayuni dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa

17:57 - April 17, 2022
Habari ID: 3475134
TEHRAN (IQNA)- Siku ya Ijumaa alfajiri, askari wa utawala haramu wa Israel waliwashambulia Wapalestina ndani ya Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds (Jerusalem) ambapo zaidi ya waumini 160 wamejeruhiwa. Jinai hiyo imewapa Wapalestina irada ya kuimarisha mapambano yao dhidi ya adui Mzayuni mtenda jinai.

Hujuma hiyo ya Wazayuni imekuja siku moja baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, kutoa wito kwa Wapalestina wajitokeze kwa wingi katika Msikiti wa Al Aqsa. Wapalestina waliitikia wito huo na Ijumaa asubuhi walijitokeza kwa wingi katika Msikiti wa Al Aqsa. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliingia kwa wingi katika Msikiti wa Al Aqsa na kuwahujumu waumini waliokuwa wamefika hapo kuswali ambapo wengi wamejeruhiwa.

Swali muhimu la kujiuliza ni hili hapa kwamba, je, ni kwa nini katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la makabiliano baina ya Wazayuni na Wapalestina?

Kwanza ni kuwa, hatua ya baadhi ya nchi muhimu za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel imepelekea Wapalestina kupoteza matumaini ya uungaji mkono wa kigeni na jambo hilo limepelekea waimarishe azma yao ya muqawama au mapambano katika kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Utawala wa Kizayuni unadhani kuwa, usalama wake utaimarika kutokana uanzishwaji uhusiano wa kawaida na tawala vibaraja za Kiarabu na hali kadhalika kadhia ya Palestina itatengwa au kusahaulika. Lakini oparesheni za vijana Wapalestina za kujitolea kufa shahidi zimeonyesha kuwa si tu kuwa kadhia ya Palestina haijasahaulika bali hivi sasa ndiyo kadhia muhimu zaidi katika eneo.

Nukta ya pili ni kuwa, Wapalestina hawana matumaini tena na Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amelaani oparesheni hizo za kujitolea kufa shahidi za wanamapamabano Wapalestina huku akiwa angali anaonyesha matumaini kuhusu mazungumzo na utawala wa Kizayuni. Mkabala wa msimamo huo dhaifu, Hamas imetangaza kuunga mkono oparesheni hizo za kujitolea kufa shahidi na ikatoa wito kwa Wapalestina kujitokeza kwa wingi katika Msikiti wa Al Aqsa kwa lengo la kuuhami msikigi huo, wito ambao uliitikiwa kwa wingi na Wapalestina siku ya Ijumaa. Nukta hiyo inaonyesha kuwa wananchi waliowengi Palestina wamefikia natija kuwa serikali ya Mamlaka ya Ndani inayoongozwa na Mahmodu Abbas haitetei maslahi ya Wapalestina na hivyo wamechukua hatua wenyewe kwa ajili ya kupambana na utawala haramui wa Israel.

Nukta ya tatu ni kuwa, Wapalestina wamefikia natija kuwa, kinyume na propaganda zinazoenezwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ni dhaifu sana kijeshi zaidi ya inavyodhaniwa. Vita vya Siku 11 vya Ghaza mwaka jana vilionyesha udhaifu mkubwa wa kijeshi wa Israel. Aidha  oparesheni za Wapalestina za kujitolea kufa shahidi katika kitovu cha utawala wa Israel pia ni ishara kuwa mfumo wa kijasusi wa utawala huo ni dhaifu mno kwani umeshindwa kutambua au kuzuia oparesheni kama hizo. Kwa kubaini udhaifu huo, Wapalestina sasa wameimarisha azma yao ya kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni kupitia mapambano.

Nukta ya nne ni kuwa, makabiliano yanayojiri yanahusu ardhi na utambulisho wa kidini wa Wapalestina na ni wazi kuwa hakuna taifa lenye fakhari linaloweza kukubali utambulisho wake huo uhujumiwe na kunyamaza kimya. Wapalestina ni watu wenye historia ndefu na pia wana utambulisho wa kitaifa na kamwe hawawezi kulinganishwa na baadhi ya nchi ndogo za Kiarabu ambazo ziliundwa na wakoloni Wamagharibi katika karne iliyopita. Hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya juu chini kuwapokonya Wapalestina utambulisho wao wa kidini yaani Msikiti wa Al Aqsa na pia utambulisho wao wa kiardhi yaani ardhi ya Palestina. Ni wazi kuwa Wapalestina kamwe hawatakubali kupokonywa utambulisho wao huo. Katika hali ambayo utawala haramu wa Israel hauna utambulisho halisi wa kitaifa na muundo wake wa kijamii ni bandia, Wapalestina wana muundo wa kijamii ulioungana na halisi na hivyo wana mshikamano katika kutetea utambulisho wao wa kitaifa.

Nukta ya mwisho ni kuwa, iwapo jamii ya kimataifa itaendelea kunyamazia kimya jinai za utawala wa Kizayuni hakuna shaka kuwa makabiliano baina ya Wapalestina na Wazayuni yatashadidi hasa wakati huu wa kukaribia Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo huadhimishwa Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

4050049

captcha