IQNA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Amani itapatikana tu nchi huru ya Palestina ikiundwa, mji mkuu wake ukiwa Quds

12:21 - April 21, 2022
Habari ID: 3475148
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema undumakuwili na kimya cha baadhi ya serikali na duru za kimataifa ndio chanzo cha kupata ubavu Israel katika kuzidisha uvamizi dhidi ya Wapalestina na ukiukaji wa haki zao.

Katika barua tofauti alizowaandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu  (OIC) Hissein Brahim Taha na pia mawaziri wa mambo ya nje wan chi za Waislamu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha wasiwasi wake kuhusu hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds (Jerusalem) na pia mashambulizi dhidi ya Wapalestina katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Amir-Abdollahian amesema ukiukaji wa maeneo matakatifu ambayo ni muhimu kwa Waislamu ni jambo linaloumiza hisia zao na halikubaliki.

Katika barua zake hizo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hujuma hizo za Israel ni ishara ya wazi kuwa utawala huo unalenga kubadilisha utambulisho wa Quds Tukufu.

Aidha amesema, "Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeliweka katika kipaumbele cha sera zake za kigeni suala la kuunga mkono ukombozi wa Palestina."

Amir-Abdollahian ametaka jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa, na hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lichukue hatua za haraka na imara za kuunga mkono Wapalestina.

Halikadhalika amesisitiza kuwa amani ya kudumu katika eneo itapatikana tu iwapo ardhi za Palestina zitakombolewa, wakimbizi wote Wapalestina warejee katika ardhi zao za jadi na taifa huru la Palestina liundwe, mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu.

3421783

captcha