IQNA

Wapigania ukombozi Palestina waitisha mkutano kujadili vitisho vya Israel

17:21 - April 13, 2022
Habari ID: 3475123
TEHRAN (IQNA)- Makundi mbalimbali ya mapambano ya Palestina yameitisha kikao cha dharura mjini Ghaza kutokana na utawala wa Kizayuni wa Israel kushadidisha jinai na vitisho dhidi ya wananchi wa Palestina.

Miji ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hasa Jenin imeshuhudia wimbi kubwa la uvamizi wa wanajeshi makatili wa Israel na hadi hivi sasa Wapalestina kadhaa wameshauawa shahidi kwa risasi za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti leo kuwa, kikao hicho cha dharura cha makundi ya muqawama ya Palestina kinafanyika leo Jumatano usiku ili kujadili jinai hizo za Wazayuni katika mji wa Jenin na dhidi ya Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Baadhi ya duru za Palestina zimeripoti kuwa, kikao hicho kimeitishwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ili kujadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa na makundi ya muqawama kukabiliana na ongezeko hilo la jinai za Wazayuni.

Kwa upande wake gazeti la Rai al Yaum limetangaza habari hiyo na kumnukuu Khalid al Batsh, mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina akisema kuwa, kikao hicho kitafanyika katika ofisi ya Khalid Sinwar, mmoja wa viongozi waandamizi wa HAMAS mjini Ghaza.

Katika upande mwingine, Muhammad Hammada, kiongozi mwingine wa HAMAS amesema, lengo la kikao hicho cha dharura ni kuchunguza njia za kujibu uvamizi na uhalifu unaofanywa na wanajeshi magaidi wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

4049037

captcha