IQNA

Ayatullah Khatami: Kuna udharura wa kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi maandamano ya Quds

18:27 - April 22, 2022
Habari ID: 3475153
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya hapa jijini Tehran amesisitizia wajibu wa kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusema kuwa, maandamano hayo yanamtia kiwewe adui.

Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, yaani Imam Khomeini MA alifanya ubunifu wa kipekee wa kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ili kuyabakisha hai milele mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Palestina.

Kona zote za Iran na Waislamu wa pembe mbalimbali za dunia na kila mpenda haki hujitokeza kuadhimisha siku hiyo kila mwaka.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami, Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema katika khutba zake za leo kwamba, kuna udharura wa kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi maandamano ya Quds mwaka huu hasa kutokana na kuongezeka vibaya jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani tena ndani ya Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Ayatullah Khatami amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa na ndoto kwamba, kwa kufikia mapatano na baadhi ya nchi za Kiarabu, ingelikuwa imelimaliza suala la Palestina na kulisahaulisha kabisa. Lakini vijana mashujaa wa Palestina wamefanya operesheni kadhaa za kujitolea kufa shahidi na kusambaratisha njama za Wazayuni na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu. Siku ya Kimataifa ya Quds kwa mwaka huu wa 1443 Hijria itakuwa Ijumaa ijayo ya tarehe 29 Aprili 2022.

4051621

captcha