IQNA

Saudia yamkamata Mpalestina aliyeomba dua ya kukombolewa Al Aqsa

18:14 - April 19, 2022
Habari ID: 3475144
TEHRAN (IQNA)- Maafisa wa usalama Saudi Arabia wamemkamata raia wa Palestina aliyekuwa akitekeleza ibada ya Umrah katika mji wa Mtakatifu wa Makka kwa sababu tu aliomba dua ya kukombolewa Msikiti wa Al Aqsa unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Mayadeen, Mpalestina huyo aliyekuwa katika Hija ndogo ya Umrah alisikika akimuomba Mwenyezi Mungu asaidie katika ukombozi wa Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) huku waumini waliokuwa karibu wakiitikia dua hiyo kwa kusema Aamyn. Kukamatwa Muislamu kwa tuhuma kama hivyo ni jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa Saudia.

Taarifa zinasema hadhirina walioitikia dua hiyo kwa kusema Aamyn nao pia walikamatwa na kusailiwa na vyombo vya kijasusi vya Saudia.

Walioshuhudua tukio hilo wanasema limejiri wakati waumini hao wakiwa katika mzunguko wa Sai baina ya Safa na Marwan na kwamba hata watoto waliokuwa hapo na kuitkia dua hiyo nao pia walikamatwa na kusailiwa. Ingawa walioitikia dua wameachiliwa huru baada ya kusailiwa lakini Mpalestina huyo bado anashikiliwa na maafisa wa usalama wa Suadia.

Ikumbukwe kuwa mwezi Februari wakuu wa Saudia walianza kuwakamata raia wa Palestina wanaoishi nchini humo ambao ilidaiwa wana uhusiano wa karibu na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas. Dkt. Muhammad Salih al-Khudri mwakilishi wa zamani wa Hamas nchini Saudia ni miongoni mwa waliokamatwa.

Baada ya Mohammad Bin Salman kuteuliwa kuwa mrithi wa Ufalme wa Saudia, kumekuwa na tetesi kuwa ufalme huo uko mbioni kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Bin Salman pia amewahi kunukuliwa akisema kuwa Israel ni muitifaki wa Saudia.

Inadokezwa kuwa Muhammad bin Salman alifanya safari za siri huko Israel ambapo alikutana na viongozi wa ngazi za juu wa utawala huo haramu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Wadadisi wa mambo wanasema hatua hizi za Riyadh zinalenga kuandaa mazingira ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, ikifuata mkumbo wa Imarati, Bahrain, Morocco na Sudan hivi karibuni zimejiunga na Misri na Jordan na kuwa nchi za Kiarabu zilizoanzisha  uhusiano wa kawaida na utawala wa Tel Aviv.

4050933

captcha