IQNA

Jinai za Israel

Sheikh Sabri akosoa mtaala uliowekwa na Israel katika shule Al-Quds

17:53 - September 20, 2022
Habari ID: 3475811
TEHRAN (IQNA) - Sheikh Mkuu wa Kipalestina Sheikh Sabri ameelezea kuunga mkono maandamano ya al-Quds (Jeruslame) inayokaliwa kwa mabavu ambayo yameitishwa kupinga mitaala ya elimu ambayo inalazimishwa na utawala haramu wa Israel katika shule za Wapalestina.

"Wazazi wa wanafunzi  Wapalestina mjini  al-Quds wana haki ya kuchagua mitaala inayoafikiana na imani, dini, kanuni na mila zao," alisisitiza Sheikh Ekrima Sabri, Mkuu wa Kamati Kuu ya Kiislamu huko al-Quds.

Sheikh Sabri ameongeza kuwa, "Wanafunzi na familia zao wametumia mgomo huo kuelezea kukataa kwao mitaala ya Israeli na kutangaza kwamba wanashikilia ule mtaala wa Palestina."

Imam huyo mkongwe alitoa wito kwa vyombo vya habari na mashirika ya Palestina na kimataifa kutetea haki ya Wapalestina ya kuamua juu ya mitaala yao wenyewe.

Takriban shule 150 za Wapalestina huko Mashariki ya al-Quds Jumatatu zilifunga milango yao kupinga majaribio ya utawala wa Israel ya kuhakiki vitabu hivyo na kulazimisha mitaala ya Kiisraeli madarasani.

Takriban wanafunzi 100,000 walijizuia kwenda shule ili kuunga mkono mgomo huo, ikiwa ni hatua ya indhari baada ya utawala haramu wa Israel kuanza kuchukua hatua za kuzilazimisha shule "kufuta simulizi za Kipalestina katika mitaala na badala yake kujumuisha simulizi za Kiyahudi ya Kiisraeli pekee.

Ziad al-Shamali, mkuu wa Umoja wa Wazazi mjini Quds Mashariki, amesema ikiwa njama za Israel zitafaulu, " utawala huo utakuwa na udhibiti wa asilimia 90 ya elimu ya wanafunzi Wapalestina mjini Al Quds."

Al-Shamali amesema wanafunzi wapatao 115,000 kutoka chekechea hadi darasa la 12 wanahudhuria zaidi ya shule 280 za Wapalestina huko al-Quds Mashariki.

Kwa miongo kadhaa, mizozo kuhusu vitabu vinavyotumiwa na shule za Wapalestina huko al-Quds Mashariki imekuwepo kati ya pande hizo mbili. Wapalestina wanaukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuingilia vitabu vyao vya masomo sambamba na kuwazuia kupokea msaada wa kifedha kwa ajili ya elimu kutoka kwa mashirika ya kimataifa na nchi za Magharibi.

Israel ilizikalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds Mashariki katika vita vya mwaka 1967, na imezidhibiti tangu wakati huo.

3480561

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha