IQNA

Umoja wa Waislamu

Wanazuoni wa Kiislamu duniani waunga mkono Al Azhar kuhusu mazungumzo ya Shia na Sunni

18:56 - November 08, 2022
Habari ID: 3476058
TEHRAN (IQNA) – Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS) umekaribisha wito wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri wa kuimarisha umoja kati ya Waislamu ndani ya mfumo wa kanuni za Kiislamu.

“Tunakubali umoja katika Umma wa Kiislamu kwa kuzingatia kanuni. Hili ni jukumu la kidini na ni Wajib (kitendo cha lazima), Katibu Mkuu wa IUMS  Sheikh Dkt. Ali Mohyiddeen Al-Qaradaghi  amesema.

"Hata hivyo, umoja huu unahitaji mazingira yanayofaa," aliongeza.

"Nchi zote za Kiislamu zina wajibu na majukumu (katika suala hili) na njia sahihi ni kwa wote kufanya mazungumzo na kuchukua hatua za dhati za kulifanikisha hili."

Ameashiria wajibu wa nchi za Kiarabu kuhusiana na suala hilo na kusema iwapo hatua zinazofaa zitachukuliwa, umoja wa Kiislamu hivi karibuni utadhihirika, kwa hiari ya Mwenyezi Mungu.

Sheikh al-Qaradaghi ameongeza kuwa anaunga mkono mwaliko wowote wa umoja kati ya Waislamu na pia umoja wa binadamu kwa ajili ya kuishi pamoja kwa amani.

Akizungumza siku ya Ijumaa nchini Bahrain, Shekhe Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar mjini Cairo Sheikh Ahmed al-Tayyib alisema: “Mimi na wanazuoni wakubwa wa Al-Azhar na Baraza la Wazee wa Kiislamu tuko tayari kwa mikono miwili kuketi pamoja kwenye meza moja ya duara na ndugu zetu wa Kishia ili kuweka kando tofauti zetu na kuimarisha umoja wetu wa Kiislamu.”

Mazungumzo hayo, alisema, yatalenga kufukuza  chuki, uchochezi na kutengwa na kuweka kando migogoro ya zamani na ya sasa.

"Natoa wito kwa ndugu zangu, wanazuoni wa Kiislamu, kote ulimwenguni wa kila itikadi na madhehebu kufanya mazungumzo ya Kiislamu," al-Tayyib alisisitiza.

Kongamano hilo lilifanyika Manama na kuhudhuriwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ambaye alifanya safari yake ya kwanza kabisa katika eneo la Ghuba ya Uajemi wiki hii.

Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu (WFPIST) yenye makao yake Tehran pia nayo imekumbatia wito wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar wa kuanzisha mazungumzo kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Sunni.

Katibu Mkuu wa WFPIST Hujjatul Islam Hamid Shahriari amemuandika barua Shekhe Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar mjini Cairo Sheikh Ahmed al-Tayyib, amekaribisha wito wa marehemu wa kufanya mazungumzo.

"Kauli yako ya utayari wa kuandaa mazungumzo haya pamoja na kushirikisha wanazuoni wa Al-Azhar inaonyesha utayari wako katika suala hili na kwamba unatafuta kufikia malengo haya kwa uaminifu na nia safi na kwa lengo la kumwendea Mwenyezi Mungu," Hujjatul Islam Shahriari aliandika.

3481175

captcha