IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu Ufaransa

Mmiliki wa mgahawa Ufaransa atozwa faini kwa kuwabagua Waislamu

11:06 - December 01, 2022
Habari ID: 3476178
TEHRAN (IQNA) - Mahakama moja ya Ufaransa imemtoza faini mmiliki wa mgahawa kusini-magharibi mwa nchi hiyo ya Ulaya kwa kumkataza mwanamke Mwislamu kuingia akiwa amevaa mtandio wa Kiislamu, unajulikana pia kama Hijabu.

Mahakama katika mji wa Bayonne katika eneo la Basque iliamua kwamba mmiliki wa mgahawa wa kike mwenye umri wa miaka 64 alikuwa na hatia ya ubaguzi wa kidini kwa kumtaka mteja avue Hijabu yake.

Tukio hilo lilitokea katika Siku ya Akina Mama mnamo Julai, wakati mwanamke huyo Mwislamu alienda kwenye mgahawa kula chakula cha jioni na mwanawe.

Picha zilizopatikana wakati wa kisa hicho zinaonyesha mama na mwanawe wakifika kwenye mlango wa mgahawa, na mwanamke anayemiliki biashara hiyo alisema hatawaruhusu wateja hao wawili kuingia kwenye mgahawa huo kwa sababu mama amevaa "Mtandio ambao ni wa Enzi za Giza."

Mmiliki wa mgahawa alidai kuwa "mtandio ni chombo cha kuwatiisha wanawake" na hivyo akamzuia mteja huyo Mwislamu kuingia.

Mteja huyo ambaye alieleza kushangazwa na maneno yaliyoelekezwa kwake, alikwenda kituo cha polisi na kuwasilisha malalamiko yake na kusema amebaguliwa.

Kutekelezwa kwa sheria zinazowalenga Waislamu nchini Ufaransa, mashambulizi ya chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi dhidi ya wanawake waliovalia Hijabu, Waislamu na taasisi za Kiislamu na maeneo ya ibada yameongezeka, jambo ambalo linaonekana kutia moyo mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya Waislamu.

Hivi majuzi, uamuzi wa manispaa ya Grenoble kuruhusu nguo za kuogelea zenye stara ambazo ni maalumu kwa wanawake Waislamu  ulisitishwa na mahakama kutokana na maagizo ya Waziri wa Mambo ya Ndani Gerald Darmanin.

3481482

Kishikizo: Hijab ، ufaransa ، waislamu
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha