IQNA

Kumbukizi ya Shahidi Soleimani

Rais wa Iran asisitiza kuhusu ulipizaji kisasi cha damu ya Shahidi Soleimani

18:22 - January 03, 2023
Habari ID: 3476349
TEHRAN (IQNA)-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Wamarekani wanapaswa kujua kwamba watu wa Iran hawataiacha damu ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani iende burE, na bila shaka watalipiza kisasi kwa damu ya shahidi huyo wa ngazi ya juu.

Kwa mujibu wa IRNA, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyed Ebrahim Raisi, ameyasema hayo leo Jumanne katika hadhara kubwa ya kuadhimisha mwaka wa tatu wa kuuawa shahidi Hajj Qassem Soleimani. Katika hotuba aliyoitoa katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini (MA) mjini Tehran, Rais wa Iran ameongeza kuwa, kuwepo watu wenye nia ya mageuzi na wanaotafuta haki ni sababu ya kuokoka na ushindi na kuongeza kuwa : "Jenerali Soleimani alikuwa mtu ambaye hafikirii tu kuhusu taifa la Iran bali pia kuhusu mataifa ya Kiislamu duniani."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na makundi mbalimbali ya watu, familia za mashahidi, mashujaa wa vita, wageni wa kimataifa, mabalozi wa nchi, viongozi wa ngazi za juu wa kitaifa na kijeshi na shakhsia wa kimataifa ameongeza kuwa: "Kumuenzi Shahidi Soleimani, ambaye ni nembo ya kimataifa ya mapambano dhidi ya madola yenye kiburi na ugaidi na kutukuza matendo yote mema  ni tangazo la chuki  na upinzani dhidi ya ukandamizaji na mfumo wa kibeberu duniani."
Raisi alisema: "Ujumbe wa kuhudhuriwa kumbukizi ya Jenerali Soleimani kwa wanaume na wanawake wote walio huru ni kwamba lazima tusimame na kupinga madola yenye kiburi na ukandamizaji na kuziba njia ya madhalimu."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Shahidi Soleimani alivunja haiba ya Marekani duniani na kuongeza kuwa: Shahidi Soleimani aliweza kuhuisha utambulisho wa Kiislamu katika eneo hili.
Aidha Rais wa Iran ameihutubu Marekani na maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kusema: Kama vile Jenerali Soleimani alivyosimama dhidi ya kujitakia makuu, dhulma, ubabe na kiburi na kuunda muqawama na mapambano katika eneo, hivi leo vijana wapenzi wa Iran watasimama dhidi ya maadui hadi mwisho.
Lt. Jenerali Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Naibu Kamanda Jeshi la Kujitolea la Wannachi wa Iraq (PMU) Abu Mahdi al-Muhandis, na wanamapambano wenzao waliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mapema  Januari 3, 2020. Shahidi Soleimani alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.

Ikulu ya White House na Pentagon ilitangaza kuwa ilihusika na mauaji hayo ya kigaidi  na kuthibitisha kuwa shambulio hilo lilitekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa Marekani wa wakati huo Donald Trump.

Mipango mbalimbali imepangwa kuandaliwa nchini Iran, Iraq na nchi nyingine kadhaa ili kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kishahidi cha Jenerali Soleimani, al-Muhandi na wanajihadi wenzao.

4111943

captcha