IQNA

Waislamu Marekani

Jiji la Minneapolis Marekani kuruhusu adhana kwa vipaza sauti mara tano kwa siku

11:41 - April 15, 2023
Habari ID: 3476872
TEHRAN (IQNA) – Jiji la Minneapolis limekuwa jiji la kwanza kubwa la Marekani kuruhusu utangazaji bila vikwazo wa wito wa Waislamu wa Sala yaani Adhana kwa sauti inayosikika nje ya msikiti mara tano kwa siku mwaka mzima.

Siku ya Alhamisi, Halmashauri ya Jiji la Minneapolis ilipiga kura kwa kauli moja kurekebisha sheria ya kelele ya jiji, ambayo ilikuwa imezuia adhana za Alfajiri na Ishaa wakati fulani wa mwaka kwa sababu zilitokea nyakati za siku wakati vizuizi vikali vya kelele vimewekwa.

"Katiba hailali usiku," alisema Jaylani Hussein, mkurugenzi mtendaji wa tawi la Minnesota la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR), baada ya kura hiyo.

Kura ya Alhamisi, wakati wa mwezi mtukufu wa Waislamu wa Ramadhani, ilionyesha msingi wa juhudi za miaka mingi za kuruhusu adhana kwa vipaza sauti huko Minneapolis, ambayo idadi ya wahamiaji wa Afrika Mashariki inayoongezeka imepelekea misikiti kuenea kila mahala.

Wajumbe watatu wa Halmashauri ya Jiji la Minneapolis - Aisha Chughtai, Jeremiah Ellison na Jamal Osman - wanajitambulisha kuwa Waislamu. "Katika kundi la 13, hilo ni kundi lenye ushawishi," Ellison alisema kabla ya kura 12-0 ya kuidhinisha Adhana kwa vipaza sauti.

Sio tu kwamba baraza lilipiga kura kwa kauli moja, uamuzi huo haukupingwa na jamii yoyote katika jiji hilo. Meya Jacob Frey anatarajiwa kutia saini hatua hiyo ndani ya wiki moja.

"Minneapolis imekuwa jiji la dini zote," alisema Imam Mohammed Dukuly wa msikiti wa Masjid An-Nur huko Minneapolis, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi kadhaa wa Kiislamu walioshuhudia kura katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Minneapolis.

Alisema ujumbe wa adhana - "Allahu Akbar," au "Mungu ni mkubwa" - unabeba ujumbe zaidi ya imani maalum za Uislamu.

Mjumbe wa Halmashauri ya Jiji la Minneapolis Lisa Goodman, ambaye siku ya Alhamisi alikuwa anaadhimisha siku ya mwisho ya Pasaka, alibainisha kuwa mwito wa Wayahudi kwa maombi - ambao kwa ujumla huzungumzwa badala ya kutangazwa - haukabiliwi na vikwazo vya kisheria. Waangalizi walibaini kuwa kengele za kanisa pia si marufuku.

3483195

captcha