IQNA

Waislamu Ulaya

Wanazuoni wa Kiislamu wa Ufaransa wa matamshi ya waziri kuhusu 'Ugaidi wa Kiislamu'

15:53 - May 25, 2023
Habari ID: 3477041
TEHRAN (IQNA) - Kundi la wanazuoni na taasisi za Kiislamu nchini Ufaransa wamekashifu vikali shutuma zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ya Ulaya dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa.

Wakati wa ziara yake nchini Marekani Ijumaa iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin alidai "kurejeshwa" kwa tishio la kigaidi barani Ulaya, akisema, "Tumekuja kuwakumbusha [Marekani] kwamba kwa Wazungu na kwa Ufaransa hatari kuu ni ugaidi wa Waislamu wa Kisunni na kwamba ushirikiano wa kupambana na ugaidi kati ya idara za kijasusi ni muhimu kabisa."
Matamshi hayo yamezua taharuki kubwa miongoni mwa Waislamu nchini Ufaransa. Kundi la wanazuoni na taasisi za Kiislamu pia lilitoa taarifa ya pamoja kukemea matamshi hayo.
"Tamko hilo la chuki si ngeni kwa waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa au maafisa wa serikali wa sasa, lakini ni hatua ya makusudi ambayo inalenga kuutukana Uislamu kwa njia isiyo ya haki," taarifa hiyo imesema.
Jambo jipya katika kauli hizi za hivi karibuni ni kuwalenga Wasunni kwa "upotoshaji na kashfa", wakati Waislamu wengi duniani ni Wasunni, iliongeza.
Kwa kauli hizi za "uchokozi na uchochezi" zinazohusisha Uislamu na Waislamu kwa ujumla na ugaidi, waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa anaonyesha "mtazamo wake wa upendeleo na upeo finyu wa kisiasa".
Katika taarifa hii, inatahadharishwa kuwa jaribio la kuwatenga Waislamu na jamii nyingine ya Wafaransa na kutumia undumakuwili linalenga kuweka vizuizi vya kisaikolojia ili kuzuia maingiliano kati ya dini tofauti na Uislamu.
Wanazuoni wa Kiislamu waliwaalika wasomi wa kisiasa wa Ufaransa kuweka kando kiburi cha kitamaduni katika kushughulika na Waislamu na kuheshimu dini ya Uislamu na imani na maadili yake, wakisisitiza kwamba uwepo wa Uislamu nchini Ufaransa ni uwepo "halali na wa kudumu".
Serikali ya Ufaransa, inayoongozwa na Macron, imeshutumiwa kwa chuki dhidi ya Uislamu na mateso dhidi ya Waislamu kwa kisingizio cha kutokuwa na dini na kupinga ugaidi. Darmanin alisaidia kupitisha sheria ya 2021 ya "kupinga utengano", ambayo wanaharakati wanasema inalenga Waislamu na inaharamisha Uislamu katika mashirika ya kiraia. Mtazamo wa serikali ya Ufaransa umekosolewa kwa kukosa kuchochea misimamo mikali huku ikidai kupambana nayo.
 
4143049

captcha