Sheikh Maher al-Muaiqly, ambaye pia msomaji mashuhuri wa Qur'ani Tukufu, alipoteza sauti katikati ya swala hiyo iliyorushwa moja kwa moja na televisheni ya taifa.
Nafasi yake ilichukuliwa na imamu mwingine, Abdul Rahman al-Sudais, ambaye aliendelea kusalisha na hivyo ibada hiyo muhimu haikusitishwa.
Mamlaka ya kidini ya Msikiti Mkuu ilisema kwamba Sheikh Muaiqly alikuwa akisumbuliwa na "uchovu" na hakuweza kumaliza sala. Imedokezwa kwamba sasa anahisi nafuu.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari cha eneo hilo, shinikizo la damu la Sheikh Muaiqly lilishuka kutokana na joto la juu la Makka, ambalo lilifikia nyuzi joto 44 mwendo wa saa saba mchana wakati wa Sala ya Ijumaa.
Ofisi ya Misikiti Miwili Mitakatifu ya Makka na Madina, imetoa taarifa kuptia mitandao ya kijamii isemayo: "Ewe Mwenyezi Mungu mlinde na mjaalie afya njema Sheikh Maher Al Muaiqly ambaye hakuweza kuendelea na Sala ya Ijumaa katika Masjid Al Haram na kupelekea Sheikh Sudais kuchukua nafasi yake."
Sheikh al-Muqaiqly ambaye ni mwanazuoni wa Fiqhi na Sharia aliteuliwa kuwa mmoja wa maimamu katika Msikiti Mkuu mwaka wa 2007, akiongoza Sala za usiku wa Ramadhani na khutba za Ijumaa katika eneo takatifu zaidi kwa Waislamu tangu wakati huo.
3484727