IQNA

Makumbusho ya Qur'ani Makkah yaonesha hati adimu

15:08 - June 09, 2025
Habari ID: 3480811
IQNA – Maonesho ya kudumu katika Makumbusho ya Qur'ani jijini Makkah yanawapa wageni tajiriba ya kipekee ya kiutamaduni na kiroho kupitia hati nadra za Qur'ani na nakala kubwa zaidi ya Qur'ani duniani.

Maonesho hayo ya kudumu, yakionyesha baadhi ya hati za Qur'ani zilizo adimu kabisa pamoja na nakala kubwa kuliko zote za Qur'ani duniani, sasa yako wazi kwa umma katika Makumbusho ya Qur'ani mjini Makkah.

Makumbusho haya yapo katika Eneo la Utamaduni la Hira karibu na Jabal al-Nour, mlima ambapo wahyi wa kwanza wa Qur'ani uliteremshwa. Katika kipindi hiki cha Hija, yamekuwa yakivutia wageni kutoka kona mbalimbali za dunia.

Makumbusho haya, ambayo yalizinduliwa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani uliopita, yanaendeshwa na Kampuni ya Samaya. Lengo la maonesho ni kuwapa wageni safari ya kielimu inayogusa nyoyo, kupitia historia ya Qur'ani, kwa kutumia mkusanyiko wa hati za kale na maonyesho ya kiingiliano.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Samaya, Fawwaz bin Abdullah Al-Muharrij, alisema makumbusho hayo yanatoa “muhtasari mpana wa mbinu za kuandika na kuhifadhi Qur'ani.” Aidha aliongeza kuwa yana “nakala kubwa zaidi ya Qur'ani duniani, inayowekwa kwenye ukumbi maalum, sambamba na nakala za zamani zinazodhihirisha mabadiliko ya hati ya Qur'ani katika karne tofauti.”

Pia, kuna vielelezo vya elimu ikiwa ni pamoja na mfano wa Pango la Hira, unaomwezesha mgeni kuona kwa macho mazingira ya awali ya ufunuo wa Qur'ani. Hati za kihistoria zinaoneshwa katika kumbi zenye teknolojia ya kisasa ili kuimarisha uelewa na mshikamano wa kiroho.

Mmoja wa wageni, Abdul Basit, alitoa shukrani kwa juhudi hizo, akisema maonesho hayo “yanasaidia kuimarisha uelewa wa wageni kuhusu umuhimu wa Qur'ani” na akalisifia jukumu la makumbusho hilo katika kuimarisha maadili ya Kiislamu.

Fahd Al-Sharif, mkurugenzi wa Eneo la Utamaduni la Hira, alisema makumbusho hayo “yanakaribisha wageni wote” na yanalenga kuimarisha tajiriba ya kiutamaduni na kidini kwa wanaozuru mji wa Makkah.

4287150

captcha