IQNA

Wanazuoni Mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiislamu /29

Tafsiri ya Qur'ani ya asiyekuwa Mwislamu kwa Kijapani

22:05 - September 20, 2023
Habari ID: 3477625
TEHRAN (IQNA) – Qur'ani Tukufu imetafsiriwa kwa lugha ya Kijapani mara kadhaa, mojawapo ikiwa tarjuma ya Okawa Shumei, ambaye si Muislamu.

Tafsiri hiyo ilichapishwa chini ya jina "Qur'an" miaka mitano baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya dunia mnamo Februari 1950.

Ilichapishwa katika kurasa 863 na Iwanami Shoten Publishers.

Okawa alizaliwa katika eneo la Yamagata kaskazini mwa Japani mwaka wa 1886. Alipokuwa akisoma falsafa katika Kitivo cha Fasihi cha Chuo Kikuu cha Tokyo, alipata ujuzi wa mawazo ya Mashariki na falsafa ya Kihindu.

Aliandika kazi tofauti za fasihi na alijulikana kama mtaalamu wa mawazo na itikadi za watu wa Japani.

Okawa pia alikuwa mtafiti makini katika uwanja wa sheria na alipata Shahada ya Uzamivu au PhD ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Tokyo.

Ni wazi kutokana na maandishi yake kwamba katika miaka yake ya shule, alisoma kwa kina kuhusumaisha ya Mtume Muhammad (SAW) na kuchukua kozi kuhusu Uislamu. Kilichochochea shauku yake ya kuusoma Uislamu ni kusoma kazi za mshairi Mjerumani Johann Wolfgang von Goethe, kama anavyoonyesha katika utangulizi wa tafsiri yake ya Qur'ani Tukufu.

Baada ya hapo, aliendelea kusoma kuhusu Uislamu hadi mwisho wa maisha yake.

Okawa alianza kutafsiri Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 30. Tafsiri yake ya sura za Qu'ran hadi Surah At-Tawbah ilichapishwa katika jarida moja la ndani ya nchi.

Wakati huo huo, alikitafsiri kitabu Al-Hadith na kuandika wasifu wa Mtukufu Mtume (SAW). Mnamo 1942 alichapisha kitabu kilichoitwa "Utangulizi wa Kuujua Uislamu" kwa Kijapani.

Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, aliamua kutafsiri Qur'ani nzima na akatumia miaka miwili katik shughuli hiyo muhimu.. Alichapisha tafsiri au tarjuma hiyo mnamo 1950.

Ingawa alisoma sana kuhusu Uislamu na kumpenda sana Mtukufu Mtume (SAW), inasemekana Okawa hakuukubali Uislamu maishani na alifariki mnamo 1959 akiwa na umri wa miaka 71.

Okawa alikuwa na ustadi wa lugha kadhaa za kigeni lakini hakuwa na ujuzi mwingi wa Kiarabu. Aliwahi kuandika katika maelezo kwamba ni Mwislamu mchamungu mwenye ujuzi kamili wa lugha ya Kiarabu ndiye anayeweza kuitafsiri Qur'ani Tukufu inavyostahiki.

Kishikizo: Wanazuoni Mashuhuri
captcha