IQNA

Kimbunga cha Al Aqsa

Ayatullah Khamenei: Licha ya Marekani kuunga mkono uhalifu wa Wazayuni, ushindi utakuwa upande wa taifa la Palestina

21:31 - October 25, 2023
Habari ID: 3477788
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Licha ya uungaji mkono wa watu waovu wa dunia na ushiriki wa Wamarekani katika uhalifu wa Wazayuni, ukatili na jinai hizi hatimaye hazitafua dafu, na katika kadhia hii na nyinginezo zijazo, ushindi utakuwa upande wa taifa la Palestina.

Ayatullah Ali Khamenei, ameyasema hayo leo Jumatano katika kikao na washiriki wa kongamano la kumbukumbu ya mashahidi 6,555 wa mkoa wa Lorestan, magharibi mwa Iran. Amegusia dhulma inayokabiliwa na subira na ukakamavu wa wananchi Wapalestina katika Ukanda wa Gaza dhidi ya jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: Utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, ambao ni utawala  uliojeruhiwa na kudhoofika, unalipiza kisasi kwa kipigo barabara cha wapiganaji wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza.

Ayatullah Khamenei ameyataja matukio ya sasa ya Gaza kuwa yanajenga mustakbali. Ameashiria dhulma zinazokabiliwa na ukakamavu wa watu wa Gaza na kusema: "Adui nduli na mfyonza damu za watu hajui mipaka ya aina yoyote katika kutenda jinai na mauaji ya watoto, wanaume, wanawake, wazee na vijana; na watu wa Gaza wanadhulumiwa kwa maana halisi ya neno hilo.”

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena amekitaja kipigo cha Jumamosi tarehe 7 Oktoba 2023, cha wapiganaji wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel kuwa ni kipigo cha maamuzi ambacho hakijawahi kushuhudiwa na akasema: Kadiri muda unavyosonga mbele, athari zisizoweza kurekebishwa za kipigo hicho zinazidi kudhihirika. 

Amesema safari za mara kwa mara za marais wa Marekani na nchi nyingine za shari na dhalimu kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani huko katika ardhi za Palestina zinazoikalia kwa mabavu ni jaribio la kuzuia kusambaratika utawala huo ghasibu na kuongeza kuwa: Watawala waovu duniani wanaona kuwa utawala wa Kizayuni "unaelekea kuusambaratika na kutoweka" kutokana na pigo kali na la wapiganaji wa Palestina; Kwa sababu hii, wanafanya safari na kuonyesha mshikamano wao na na Wazayuni na kuwapa zana za kutendea uhalifu kama mabomu na silaha nyinginezo, katika jaribio la kuubakisha hai kwa nguvu utawala uliojeruhiwa na kuatilika.

Ayatullah Ali Khamenei ameitaja Marekani kuwa ni mshirika halisi katika uhalifu unaofanywa na watendajinai wa Kizayuni na amesisitiza kuwa: Mikono ya Wamarekani imejaa damu za watoto, wanawake na mashahidi wengine wa Gaza hadi kwenye vifundo vya mkono, na kwa hakika Wamarekani ndio wanaosimamia uhalifu huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kutikisika kwa dhamiri ya umma wa walimwengu huko Amerika, Ulaya, nchi za Kiislamu na kanda nyingine za dunia kuwa ni jibu kwa kiwango na kina cha jinai za mara kwa mara za utawala wa Kizayuni wa Isarel dhidi ya watu wa Palestina. Ameongeza kuwa: Wale wanaodai kutetea uhuru na haki za binadamu barani Ulaya wamepiga marufuku maandamano ya kuwatetea Wapalestina, lakini watu wamepuuza marufuku hiyo, na wanamiminika mitaani na kutangaza hasira na ghadhabu zao, na hakuna mtu atakayeweza kuzuia majibu ya mataifa dhidi ya ukatili wa Wazayuni.

3485743

Habari zinazohusiana
captcha