IQNA

Ayatullah Khamenei: Mpango wa kijinga wa Marekani kuhusu Gaza haufiki popote

20:42 - February 18, 2025
Habari ID: 3480233
IQNA-Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akiwapongeza wapiganaji wa Muqawama kwa ushindi wao katika Ukanda wa Gaza, amesisitiza kwamba kazi kubwa ya viongozi na wapiganaji wa Muqawama wa Palestina ipo katika "umoja na mshikamano" na "kusimama imara" dhidi ya adui, kuendesha mchakato mgumu wa mazungumzo, pamoja na uvumilivu na ustahimilivu wa wananchi, ambavyo vimeinua heshima ya Muqawama katika eneo.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Ofisi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, siku ya Jumanne alipokutana na Ziyad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati Jihad Islami ya Palestina na ujumbe wake, aliutaja ushindi wa Muqawama wa Kiislamu na wananchi wa Gaza dhidi ya utawala wa Kizayuni na Marekani kuwa wa kihistoria. Aidha, alisisitiza kuwa ushindi huo umeweka kiwango kipya katika harakati za mapambano ya Muqawama.

Ayatullah Khamenei amezungumzia baadhi ya mipango ya kijinga ya Marekani pamoja na baadhi ya mipango mingine kuhusu Ukanda wa Gaza na Palestina, akisema: "Mipango hii haitafika popote. Wale waliodai mwaka mmoja na nusu uliopita kwamba wataangamiza Muqawama katika muda mfupi sasa wanajikuta wakikabidhi mateka wao kwa vikundi vidogo vya wapiganaji wa Muqawama huku wakilazimika kuachilia idadi kubwa ya wafungwa wa Kipalestina."

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kuwa mbinu ya Muqawama ya  kuachilia mateka wa Kizayuni inaonesha hadhi na nguvu ya Muqawama mbele ya macho ya dunia. Ameongeza kuwa hivi sasa fikra za umma wa dunia zinaelekea kuunga mkono Palestina, na katika mazingira haya, hakuna mpango wowote utakaofaulu bila ridhaa ya Muqawama na wananchi wa Gaza.

Kwa upande wake, Ziyad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Jihad ya Kiislamu ya Palestina, amempongeza Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ushindi mkubwa wa Muqawama huko Gaza. Ameeleza kuwa ushindi huo umetokana na msaada wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na uongozi wa shahidi Sayyid Hassan Nasrallah.

Amebainisha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, muqawama wa Palestina ulikuwa unapambana moja kwa moja na Marekani na nchi za Magharibi. Aidha amesema pamoja na kutokuwepo mlingano wa kijeshi, Muqawama wa Palestina uliweza kupata ushindi mkubwa.

Ameongeza kuwa mshikamano wa kisiasa na wa kivita kati ya makundi ya Muqawama wa Kipalestina na wa Kilebanoni ulikuwa miongoni mwa sababu kuu za ushindi wa Gaza. Pia, ametoa taarifa kuhusu matukio ya hivi karibuni huko Gaza, Ukingo wa Magharibi, pamoja na mchakato wa mazungumzo na makubaliano yaliyofikiwa. Amesisitiza kuwa njia ya Muqawama haitasahaulika kamwe, na wapiganaji wa Muqawama wataendelea kuifuata njia hiyo.

4266977

Habari zinazohusiana
captcha