IQNA

Kimbunga cha Al Aqsa

UNICEF 'Yashtushwa' na idadi ya watoto waliouawa katika vita vya Israel dhidi ya Gaza

11:58 - October 26, 2023
Habari ID: 3477791
AL-QUDS (IQNA) - Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema hadi sasa takriban watoto 2,360 walikuwa wameuawa katika mashambulizi ya anga ya  utawala wa Israel huko Gaza, na kubainisha masikitiko yake kuhusu idadi "ya kushtua" ya watoto waliojeruhiwa katika eneo hilo lililozingirwa.

Ikiripoti kuwa watoto 2,360 wameuawa katika muda wa chini ya wiki tatu, UNICEF imetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na upatikanaji endelevu na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu.

Watoto wengine 5,364 huko Gaza wamejeruhiwa katika "mashambulizi yasiyoisha," UNICEF iliongeza Jumanne. Zaidi ya watoto 400 wanaripotiwa kuuawa au kujeruhiwa kila siku katika eneo la Palestina lililozingirwa, ilisema UNICEF.

Tarehe 7 Oktoba, harakati ya mapambano ya Kiislamu (muqawama al Islamiya) ya Palestina, Hamas, ilianzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu ambayo yamepachikwa jina bandia la Israel. Jeshi la utawala haramu wa Israel tangu wakati huo limeshambulia kwa mabomu Gaza na kuua takriban watu 6,000. Watoto ni takriban asilimia 50 ya wakazi wa Gaza wapatao milioni 2.3.

"Hali katika Ukanda wa Gaza ni doa linaloongezeka kwenye dhamiri zetu za pamoja. Kiwango cha vifo na majeraha ya watoto kinashangaza,” alisema Adele Khodr, mkurugenzi wa UNICEF wa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Ukosefu mbaya na unaoendelea wa maji pia unaleta madhara makubwa kwa watoto, UNICEF ilisema Jumanne, ikibainisha kuwa mifumo mingi ya maji imeathirika sana au haifanyi kazi kutokana na uhaba wa mafuta na uharibifu wa miundombinu muhimu.

UNICEF imesema mafuta ya petroli na diseli, ambayo Israel haijaruhusu kuingia Gaza, ni ya umuhimu mkubwa kwa uendeshaji wa vifaa muhimu kama vile hospitali, mitambo ya kusafisha maji ya baharini na mabomba ya maji. Pia ilisema vitengo vya wagonjwa mahututi vya watoto wachanga, na watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati walio katika inkubeta, hutegemea uingizaji hewa wa mitambo, na  hivyo umeme sasa ni suala la maisha na kifo.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: Hali katika Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) inazidi kuwa mbaya na huenda vita vya Gaza vikaenea katika eneo hilo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu Gaza jana Jumanne kwamba kwa bahati nzuri, baadhi ya misaada imefika Gaza. Katika kikao hicho cha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa kuwalinda raia haimaanishi kuamuru kuhamishwa kwa zaidi ya watu milioni moja huko kusini mwa Ukanda wa Gaza na kuendeleza mashambulizi ya mabomu kusini mwa eneo hilo.

Ili kufidia kushindwa kwake  baada ya kupata kipigo  utawala wa Kizayuni umeamua kuwaua raia na wananchi madhulumu wa Palestina, na hadi sasa umewauwa shahidi Wapalestina zaidi ya elfu nne wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake katika mashambulizi na hujuma za kikatili dhidi ya nyumba za raia, vituo vya  matibabu, misikiti na maeneo ya kuwahifadhi wakimbizi wa Kipalestina huko Ghaza.

3485742

Habari zinazohusiana
captcha