IQNA

Watetezi wa Palestina

Sisitizo kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kufichua jinai za Israel

22:13 - May 12, 2024
Habari ID: 3478806
IQNA - Kongamano lililopewa jina la "Muqawama (Mapambano) na Vyombo vya Habari vya Wapalestina" limefanyika katika Taasisi ya Ittila'at mjini Tehran ambapo wazungumzaji walisisitiza nafasi ya vyombo vya habari katika kuangazia jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Mwanafikra na mwandishi wa Palestina Munir Shafiq na wataalamu kadhaa wa kisiasa, vyombo vya habari na kitamaduni walihudhuria kongamano hilo siku ya Jumamosi.

Abbas Khameyar, mkuu wa masuala ya kitamaduni na kijamii wa Chuo Kikuu cha Dini na Madhehebu, alikuwa mmoja wa wazungumzaji waliosema kwamba kutokana na Operesheni ya Kimbuga cha Al-Aqsa ambayo jeshi la muqawama wa Palestina liliifanya dhidi ya utawala wa Kizayuni Oktoba 7 mwaka jana, jinai za Israel zimefichuliwa kwa ulimwengu.

Kabla ya hapo, Wazayuni walikuwa wakijifanya kuwa wasio na hatia lakini tangu Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, jinai zao nyingi zimerekodiwa kwenye eneo la tukio kutokana na utayari wa vyombo vya habari vya muqawama, alisema.

Khameyar alibainisha kuwa vyombo vya habari vya upande wa muqawama kama vile Al-Alam, Al-Mayadeen, Al-Ahed, na Al-Manar vilichukua nafasi kubwa katika kuongeza ufahamu kuhusu ukatili wa Israel.

Naye mtaalamu wa masuala ya  Mashariki ya Kati Mohammad Ali Muhtadi alipanda jukwaa na kusema kwamba tangu Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, utawala wa Kizayuni umekabiliwa na kushindwa kwa kijasusi na kijeshi na haujaweza kufidia kushindwa huko.

Leo, sura ya kweli ya utawala wa Israel imefichuliwa baada ya utawala huo kuficha sura yake ya kikatili na mbaya kwa miaka, alisema.

Aidha amesisitiza kuwa, kuuawa shahidi maelfu ya Wapalestina katika mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza hakutakuwa bure bali damu yao itabadilisha milingano ya kieneo na kimataifa.

Munir Shafiq katika hotuba yake ameashiria kushindwa utawala wa Kizayuni katika lengo lake la kuangamiza harakati ya muqawama ya Hamas licha ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya kinyama ya kijeshi huko Gaza.

Alisema ingawa wengi walitarajia kuona Israel ikiteka Gaza ndani ya wiki moja tu, utayari wa vikosi vya muqawama na uongozi wa Gaza ulizuia Wazayuni kufikia lengo lao.

Pia alielezea hatua ya Hamas kukubali pendekezo la hivi karibuni la kusitisha mapigano kama ishara ya nguvu yake na akasema ikiwa adui atakubali au kukataa pendekezo hilo, itamaanisha kushindwa kwa adui.

Hamas ilianzisha Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba ili kukabiliana na ukatili wa Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na ukiukaji wake wa utakatifu wa Msikiti wa Al-Aqsa.

3488299

Habari zinazohusiana
captcha