IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu apongeza msimamo wa Tunisia dhidi ya Israel

12:09 - May 23, 2024
Habari ID: 3478872
IQNA- Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyed Ali Khamenei amekaribisha kufufuliwa uhusiano kati ya Iran na Tunisia, kulikowezeshwa na ziara ya Rais Kais Saied wa Tunisia nchini Iran, na kupongeza misimamo ya nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika dhidi ya Israel.

Saied, alifika Iran Jumatano kuhudhuria hafla ya kumuomboleza Rais wa Iran Ebrahim Raisi, alikutana na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kabla ya hafla hiyo.

Ayatullah Khamenei alimshukuru Rais Kais Saied kwa hisia za udugu na za dhati kuhusiana na tukio la kufa shahidi rais wa Iran na wenzake na kusema: "Kumpoteza Rais na wenzake aliokuwa nalo ni jambo zito, lakini katika zama zote za uwepo wa Jamhuri ya Kiislamu, daima tumeona kwamba kwa kuzingatia hekima ya Mwenyezi Mungu na subira na istikama ya wananchi, matukio machungu yamekuwa chanzo cha maendeleo na harakati.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameeleza furaha yake kwa kuanzishwa upya uhusiano kati ya Iran na Tunisia kutokana na ziara ya Rais wa nchi hii na kuongeza kwamba: "Kuwepo shakhsia mashuhuri na wa kielimu kama Kais Saied  kama rais wa Tunisia kunaibua sura mpya na ni fursa kwa nchi hii baada ya miaka mingi ya utawala wa kimabavu na kujitenga na ulimwengu wa Kiislamu. 

Ayatullah Khamenei ameashiria harakati za watu wa Tunisia miaka michache iliyopita, ambazo zilikuja kuwa msingi wa harakati kubwa huko Kaskazini mwa Afrika na kumfahamisha Rais Kais Saied kwamba: "Wananchi wa Tunisia wana kipaji kikubwa cha maendeleo na kusonga mbele, na tunatumai kuwa kwa mpango wako  tutafikia umoja unaohitajika."

Akirejelea misimamo ya Rais wa Tunisia dhidi ya Uzayuni, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Misimamo hiyo inapaswa kuendelezwa katika ulimwengu wa Kiarabu, kwa sababu kwa bahati mbaya, katika ulimwengu wa Kiarabu, masuala hayo hayatiliwi maanani, na tunaamini kwamba njia pekee ya mafanikio ni istiqama."

Akizungumzia uwezo mzuri wa Iran na Tunisia katika kuendeleza uhusiano, Ayatullah Khamenei amesema: "Serikali ya marehemu rais wetu ilikuwa serikali ya kazi, harakati na uhusiano, na sasa Mohammad Mokhber ataendeleza njia hiyo hiyo ya kuendeleza uhusiano na nchi tofauti."

Katika mkutano huo, rais wa Tunisia Rais Kais Saied pia ametoa salamu za rambirambi za dhati za serikali na wananchi wa Tunisia kutokana na tukio hilo la kusikitisha la hivi karibuni na kusema: "Mkutano wetu wa mwisho na hayati rais wa Iran ulikuwa nchini Algeria miezi kadhaa iliyopita na huko tulikubaliana kwamba nitatembelea Tehran, lakini sikuwahi kufikiria kwamba ningekuja Tehran kutoa rambirambi zangu kwa kifo chake."

Akizungumzia nia ya pamoja ya nchi hizi mbili ya kupanua uhusiano katika nyanja zote, Rais wa Tunisia ameelezea matumaini yake kwamba kwa kufuata makubaliano hayo, upanuzi wa ushirikiano utafikiwa kwa njia ya kivitendo.

Kais Saied pia katika kikao hicho na Kiongozi Muadhamu ameashiria hali ya eneo na kuuawa watu wa Ghaza katika hujuma inayoendelezwa hivi sasa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kwamba: "Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuacha msimamo wake wa hivi sasa wa kutochukua hatua na badala yake kuwa na sauti moja katika kutetea haki za watu wa Palestina katika maeneo yote ya Palestina sambamba na kuundwa serikali huru ya Palestina ambayo mji wake mkuu utakuwa Quds Tukufu (Jerusalem)."

Aidha Rais wa Tunisia amebainisha kuwa: Leo hii jumuiya ya kibinadamu duniani imeipita jumuiya ya kimataifa, ambapo jumuiya ya kibinadamu katika nchi mbalimbali imejitokeza kwa sauti moja na kupinga ukatili, jinai na mauaji ya umati yanayofanywa na utawala huo wa kibaguzi huko Gaza.

 3488460

captcha