Katika makala iliyochapishwa katika tovuti ya Televisheni ya Al-Mayadeen, Hussein al-Batsh aliandika kwamba Raisi alikuwa mmoja wa marais wa Iran waliofanya juhudi kubwa zaidi kuwatetea Wapalestina na kadhia ya Palestina.
Amesema Ayatullah Raisi hakukosa fursa ya kueleza msimamo wake thabiti wa kuunga mkono haki za wananchi wa Palestina na muqawama (mapambano) yao dhidi ya adui Mzayuni.
Waziri wake wa mambo ya nje, Hossein Amir-Abdollahian, pia alitetea kwa kiasi kikubwa suala la Wapalestina katika safari zake katika nchi tofauti na mikutano na viongozi wa mhimili wa muqawama, al-Batsh alisema.
Ameitaja hotuba aliyoitoa Rais Raisi kwa njia ya video kwenye hafla iliyofanyika Ukanda wa Gaza mwezi Aprili 2023 kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds kuwa ni moja ya misimamo bora ya Raisi.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya Wapalestina huko Gaza, Ayatullah Raisi alisisitiza misimamo isiyobadilika ya Iran kuhusu uungaji mkono wa muqawama wa taifa la Palestina, alibainisha.
Wakati huo, vyombo vya habari vya Israel vilielezea hotuba hiyo kama isiyo na kifani, mchambuzi huyo wa Lebanon alisema.
Alibainisha kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kwa rais wa nchi kuhutubia moja kwa moja watu wa Gaza, eneo la Palestina ambalo limekuwa chini ya mzingiro wa kikatili tangu 2007.
Rais wa Iran pia alihusika katika juhudi za kukomesha uvamizi wa Israel huko Gaza baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyoanzishwa na vikosi vya upinzani, al-Batsh aliendelea kusema.
Vile vile aliashiria uungaji mkono wa Ayatullah Raisi kwa wanachama wengine wa mhimili wa upinzani, kutoka Lebanon hadi Yemen hadi Iraq.
Amemalizia kwa kusema kuwa, kumpoteza Rais Raisi ni hasara kubwa kwa Iran pamoja na Palestina na waungaji mkono wake.
Rais Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Amir-Abdollahian, na ujumbe walioandamana nao walipoteza maisha baada ya helikopta iliyokuwa imewabeba kuanguka katika mkoa wa kaskazini-magharibi wa Azarbaijan Mashariki mnamo Mei 19, 2024.
3488576