Kesi hiyo inalenga kubatilisha marufuku ya wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani kwa kituo hicho.
Mwanasheria wa kituo hicho alisema kwa kufunga kituo hicho na Msikiti wake wa Imam Ali (AS), wizara ya mambo ya ndani imewanyima haki Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia, ambao kwa kawaida hkusanyika hapo kwa ajili ya swala na hivyo marufuku hiuo inawazuia kutekeleza dini yao kwa uhuru.
Wakili huyo alisema mahakama ya utawala ya shirikisho huko Leipzig imethibitisha kupokea malalamiko hayo.
Wawakilishi wa Kituo cha Kiislamu cha Hamburg wamezitaja tuhuma zilizotolewa dhidi ya kituo hicho katika hukumu iliyopelekea kupigwa marufuku kwake kuwa hazina msingi.
Wizara ya mambo ya ndani ya Ujurumani ilidai kuwa kituo hicho kinaongozwa na Iran na eti kinafuatilia malengo yanayopingana na Katiba ya Ujerumani.
Polisi wa Ujerumani walivamia Kituo cha Kiislamu cha Hamburg na majengo 53 ya shirika hilo mnamo Julai 24. Polisi wa Ujerumani wanasema hilo lilichukua hatua kwa kuzingatia amri ya mahakama. Majengo yaliyovamiwa ni pamoja na vituo katika miji mingine mbali na Hamburg, kama vile Frankfurt, Berlin, na Munich.
Wizara ya Ujerumani ilidai kuwa kituo hicho kimekuwa kikiunga mkono harakati Hizbullah ya Lebanon ambayo imepigwa marufuku nchini Ujerumani.
Marufuku hiyo ya Ujerumani itasababisha kufungwa kwa misikiti minne ya madhehebu ya Shia nchini humo, ukiwemo msikiti mashuhuri wa Imam Ali (AS) ambao ni miongoni mwa misikiti mikongwe zaidi nchini Ujerumani. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1965.
Kituo cha Kiislamu cha Hamburg ni mojawapo ya vituo muhimu na vya kihistoria vya Kiislamu vya Ujerumani, vilivyoanzisha kwa uungaji mkono wa Ayatullah Boroujerdi.
Kituo hicho huchapisha majarida katika Kijerumani na Kiajemi na hutoa huduma za ushauri kwa Mashia wa Hamburg. Kituo hicho pia kinajivunia maktaba yenye mada zaidi ya 6,000 kuhusu masomo mbalimbali ya Kiislamu.
/3489516