Akihutubia kikao cha baraza hilo mjini Tehran Jumanne asubuhi, Ayatullah Mohammad Ali Movhedi Kermani alilaani vikali ukatili na jinai za utawala ghasibu wa Israel.
Amesema Marekani inadai kuwa inatetea haki za binadamu lakini inatoa zaidi ya asilimia 70 ya silaha zinazotumiwa na utawala wa Israel na kuunga mkono kikamilifu vita vya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala huo.
Mwanazuoni huyo pia ametoa pongezi kwa mashahidi wa muqawama au mapambano ya Kiislamu, akiwemo Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah, Sayed Hassan Nasrallah, afisa wa Hizbullah Sayed Hashem Safieddine, na viongozi wa Hamas Ismail Haniyeh na Yahya Sinwar, akisema damu ya mashahidi hao itaharakisha maangamizi ya utawala katili wa Israel.
Vilevile amelaani kimya cha kutisha na kutojali Umoja wa Mataifa na baadhi ya serikali hususan serikali za baadhi ya nchi za Kiislamu kwa umwagaji damu na ukatili katika Ukanda wa Gaza na Lebanon na ambao umepelekea idadi kubwa ya watu kuwa wakimbizi.
Kwingineko katika hotuba yake, Ayatullah Movahedi Kermani amewapongeza Wanajeshi wa Iran kwa kutekeleza vyema Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya Kwanza na Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya Pili dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidh amepongeza Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran kwa kufanikiwa kuzima shambulio la hivi karibuni la Israel dhidi ya nchi hiyo.
Baraza la Wanazuoni Wataalamu la Iran lina jukumu la kumchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Wajumbe wa baraza hilo huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi kuhudumu muhula wa miaka minane.
3490571